Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanajeshi wawili wa Tanzania wameuawa katika mapigano yaliyofanyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kati ya Jeshi la Tanzania na waasi wa M23.
Taarifa hiyo inasema kuwa wanajeshi hao walifariki kutokana na mfululizo wa mashambulizi yaliyofanywa na waasi wa M23 katika maeneo ya Sake na Goma.
Taarifa hiyo ilisema: "Kufuatia mashambulizi ya mfululizo katika maeneo ya Sake na Goma yaliofanywa na waasi wa M23 tarehe 24 na 28 Januari, Jeshi la Ulinzi la Tanzania (JWTZ) limewapoteza askari wake wawili na wengine wanne kujeruhiwa. Majeruhi wanaendelea kupata matibabu mjini Goma."
Taarifa hiyo ilitiwa saini na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Kanali Gaudentius Gervas Ilonda, na kuongeza kuwa taratibu za kusafirisha miili ya marehemu pamoja na majeruhi zinaendelea kupitia sekretariati ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Aidha, taarifa hiyo ilisisitiza kuwa vikosi vya wanajeshi wa Tanzania vilivyopo nchini DRC viko salama, imara, na vinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa maelekezo ya uongozi wa SADC.
Katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Mataifa ya Afrika Kusini (SADC) siku ya Ijumaa Januari 31, Mwenyekiti wa SADC, Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe, alisema kwamba hadi kufikia Januari 31, wanajeshi kutoka Malawi, Afrika Kusini, na Jamhuri ya Muungano ya Tanzania walifariki katika makabiliano na kundi la M23.
Hadi sasa, Afrika Kusini imetangaza kuwapoteza wanajeshi 14, baada ya mmoja kuthibitishwa kufariki hospitalini usiku wa Jumamosi.
SADC ilisema kuwa ingawa kikosi cha SAMIDRC kilichoanza kazi baada ya kuondoka kwa kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) hakijatimiza majukumu yake, kitengo cha usalama cha TROIKA, kinachoongozwa na Tanzania, kinatarajiwa kufanya kikao cha dharura kutafuta mbinu za kuwaleta pamoja wahusika wote kwenye mzozo wa mashariki mwa DRC ili kuhakikisha kwamba vita vinakomeshwa.
Aidha, Troika inatarajiwa kuhakikisha kwamba njia za kuingiza msaada wa kibinadamu zinafunguliwa kwa ajili ya kuwafaa waathirika wa machafuko yanayoendelea katika mji wa Goma na maeneo mengine.
Msimamo wa SADC Nchini DRC
Licha ya vikosi vya SAMIDRC kukumbwa na majeraha na maafa ya wanajeshi kutoka mataifa husika, SADC imeeleza ahadi yake ya kuendelea kusimama na DRC katika juhudi za kutafuta amani, kutetea utaifa wa DRC, na kuhakikisha usalama wa raia wa nchi hiyo.
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekuwa likishiriki katika shughuli za ulinzi wa amani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa na jumuiya za kikanda, na limekuwa likitekeleza majukumu yake katika nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Lebanon, Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Liberia, Msumbiji, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

0 Comments:
Post a Comment