Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewataka waandishi wa habari nchini kuhakikisha taaluma yao inachangia kujenga taifa, hususan kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Akizungumza katika kikao na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Msigwa amesema sekta ya habari inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani na mshikamano wa Tanzania kwa kuandika habari zenye tija na maudhui yanayochochea maendeleo ya taifa.
“Tunahitaji waandishi wa habari waandike habari zinazojenga taifa na kulinda amani. Tunajivunia sekta ya habari, tunaamini itaendelea kusaidia kuitunza amani ya nchi yetu.
Serikali ina dhamira ya kweli ya kushirikiana na wanahabari ili kuhakikisha sekta hii inakuwa mfano wa kuigwa barani Afrika,” amesema.
Ameongeza kuwa serikali inaendelea kutatua changamoto zinazowakabili waandishi wa habari, hasa nyakati za kampeni, ikiwemo suala la usafiri. “Ni muhimu waandishi wa habari kupewa magari mazuri na salama badala ya mabovu,” amesisitiza.
Aidha, amewataka wanahabari kuzingatia weledi na maadili ya taaluma yao kwa kuandika vichwa vya habari vyenye tija kwa Watanzania na kuepuka habari chochezi.
“Kuandika habari mbaya za nchi yako hakukufanyi kuwa mwandishi bora. Epukeni habari zinazoleta taharuki kwa umma, badala yake zingatieni weledi wa taaluma ili tasnia ya habari ipate heshima inayostahili,” amesema Msigwa.
Kwa mujibu wake, serikali imeanzisha utaratibu wa kuwapeleka waandishi wa habari kwenye miradi mikubwa ya maendeleo ili wapate uelewa wa kina na kutoa taarifa sahihi kwa umma.

0 Comments:
Post a Comment