TAASISI ZA UMMA ZATUNUKIWA TUZO ZA SERIKALI MTANDAO

 


Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imetoa tuzo kwa taasisi za umma zilizofanya vizuri katika utekelezaji wa serikali mtandao, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kuchochea matumizi ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi serikalini.



Akizungumza wakati wa ugawaji wa tuzo hizo katika Kikao Kazi cha 5 cha Serikali Mtandao kilichofanyika jijini Arusha, Meneja wa Usimamizi wa Udhibiti na Viwango vya Serikali Mtandao, Sultana Seiff, alisema kuwa mchakato wa utoaji wa tuzo hizo ulizingatia vigezo mbalimbali ili kubaini taasisi zilizofanya vizuri zaidi katika utekelezaji wa serikali mtandao.




“Tuzo hizi zimegawanyika katika maeneo makuu matatu, ambayo ni uzingatiaji wa Sheria ya Serikali Mtandao, viwango na miongozo (Best Performance in Compliance to e-Government Act, Standards and Guidelines); matumizi ya TEHAMA katika kuwashirikisha wananchi kupata huduma bora za serikali (Best Performance in Utilization of ICT for Citizen Engagement); na taasisi kinara katika kuunganisha na kubadilishana taarifa kupitia Mfumo wa Kubadilishana Taarifa Serikalini ujulikanao kama GoVESB (Best Performance in e-Government System Integration through GoVESB),” alisema Seiff.




Kwa upande wa taasisi zilizoshinda katika kipengele cha uzingatiaji wa Sheria ya Serikali Mtandao, viwango na miongozo, Wizara ya Katiba na Sheria iliibuka mshindi wa kwanza, ikifuatiwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika nafasi ya pili. Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) ilishika nafasi ya tatu, huku Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ikishika nafasi ya nne.


Kwa taasisi zilizo katika ngazi ya tatu ya ukomavu wa TEHAMA serikalini, Halmashauri ya Wilaya ya Geita iliibuka mshindi pekee kwa mwaka huu.


Katika kipengele cha matumizi ya TEHAMA kwa ajili ya kuwashirikisha wananchi katika kupata huduma bora za serikali, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilishika nafasi ya kwanza. 


Nafasi ya pili ilichukuliwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), huku nafasi ya tatu ikienda kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA).


Kwa upande wa taasisi zilizoibuka kinara katika kuunganisha na kubadilishana taarifa kupitia Mfumo wa Kubadilishana Taarifa Serikalini (GoVESB), Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) lilitangazwa kuwa mshindi pekee.


Seiff alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya TEHAMA serikalini ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza uwajibikaji wa taasisi za umma.

0 Comments:

Post a Comment