Teknolojia Ya Drones Yaimarisha Udhibiti Wa Wanyamapori Waharibifu Korogwe

 


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imekagua na kuridhishwa na matumizi ya teknolojia katika kituo kipya cha askari kitakachotumika kudhibiti wanyamapori waharibifu. Kituo hicho kipo katika kijiji cha Goha, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga.



Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Timotheo Mnzava, ambaye pia ni Mbunge wa Korogwe Vijijini, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutumia teknolojia ya ndege nyuki (drones) katika kufukuza wanyamapori waharibifu, hususan tembo.



"Tunaipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na taasisi zake, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), kwa kushirikiana kuhakikisha udhibiti wa wanyamapori waharibifu katika Wilaya ya Korogwe unaimarika," alisema Mnzava.




Kamati hiyo ilishuhudia zoezi la kufukuza tembo kwa kutumia ndege nyuki iliyorushwa umbali wa takribani kilomita 10 huku vipaza sauti vyake vikitoa kelele za kuwatisha wanyama hao.



Askari Uhifadhi Daraja la Tatu, Isaack Daudi kutoka Hifadhi ya Taifa Mkomazi, ambaye ni mmoja wa wataalam wa urushaji wa ndege nyuki katika TANAPA, alieleza kuwa ndege hiyo ni aina ya DJI Matrice 30 (M30) toleo la mwaka 2024.



"Ndege nyuki hii ina uwezo wa kwenda umbali wa kilomita 10 na juu mita 300. 


Pia ina teknolojia ya kipaza sauti kwa ajili ya kupiga kelele wakati wa kufukuza tembo, jambo linaloongeza ufanisi wa zoezi hilo," alisema Daudi.



Kituo hicho kilijengwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na kukabidhiwa kwa Hifadhi ya Taifa Mkomazi kwa ajili ya usimamizi. 


Kituo hicho kina askari sita, gari moja pamoja na ndege nyuki moja, vitendea kazi ambavyo vimetengwa mahsusi kwa ajili ya kufukuzia wanyamapori waharibifu.


Wananchi watanufaika na kituo hicho ambacho kitahudumia vijiji sita, ambavyo ni Manga, Mtitiro, Masira, Kwenangu, Mkomazi na Mikoche.


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilikagua kituo hicho katika mwendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii. 


Kamati hiyo iliambatana na Dunstan Kitandula, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. 


Hassan Abbas, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba, Naibu Katibu Mkuu (Maliasili) na watendaji wengine kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake.

0 Comments:

Post a Comment