Sultani Makenga: Mwanajeshi wa Vita, Kiongozi wa M23 na Mzozo Usioisha Mashariki mwa DRC

 


Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeendelea kukumbwa na machafuko ya kivita kwa miongo kadhaa, hasa katika eneo la mashariki. 


Katika siku za hivi karibuni, kundi la waasi la M23 limechukua udhibiti wa sehemu muhimu za mkoa huo, likisababisha vifo vya maelfu ya watu na kulazimisha wengine wengi kuwa wakimbizi.


Mzozo huu umeibua mvutano mkali kati ya DRC na Rwanda, ambapo serikali ya Congo inaituhumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23, tuhuma ambazo Kigali imekanusha mara kwa mara.



Ili kuelewa kiini cha vita hivi, ni muhimu kumwangalia mmoja wa wahusika wakuu wa mzozo huu – Sultani Makenga, kiongozi wa kundi la M23. 


Maisha yake yanaakisi historia ndefu ya vita, uingiliaji wa kigeni, na mvutano wa kisiasa unaotokana na rasilimali za DRC.


Maisha ya Sultani Makenga: Kutoka Masisi Hadi Ukombozi wa Kigali



Sultani Makenga alizaliwa tarehe 25 Desemba 1973 katika mji wa Masisi, mashariki mwa DRC. 


Akikulia katika familia ya Kitutsi, alikumbana na changamoto za ubaguzi dhidi ya jamii yake, jambo lililomfanya kuacha shule akiwa na umri wa miaka 17 na kujiunga na kundi la waasi wa Tutsi lililokuwa mpakani mwa Rwanda.


Kundi hilo, Rwandan Patriotic Front (RPF), lilikuwa likipigania haki za Watutsi waliokimbia Rwanda kwa sababu ya vurugu za kikabila. RPF iliongozwa na Paul Kagame, ambaye baadaye alikuja kuwa Rais wa Rwanda.


Katika kipindi cha miaka minne ya mapambano, Makenga alipata uzoefu wa vita, hasa wakati wa Mauaji ya Kimbari ya 1994, ambapo takriban Watutsi 800,000 waliuawa na wanamgambo wa Kihutu. RPF hatimaye ilishinda na kuchukua madaraka Kigali, jambo lililosababisha wafuasi wa serikali ya Kihutu kukimbilia DRC.



Akielezea uzoefu wake wa vita, Makenga aliwahi kusema:

"Maisha yangu ni vita, elimu yangu ni vita, na lugha yangu ni vita… lakini mimi ninaheshimu amani."


Baada ya ushindi wa RPF, Makenga alijiunga na jeshi la Rwanda, akapanda vyeo na kuwa naibu kamanda wa kikosi. Hata hivyo, alihisi kuwa nafasi yake katika jeshi ilikwamishwa na ukosefu wa elimu ya juu na ujuzi mdogo wa lugha ya Kifaransa na Kiingereza.

Kwa mujibu wa Rift Valley Institute, mshirika wake mmoja wa zamani alisema:

"Makenga alikuwa mzuri sana katika kuanzisha mitego na kupanga mashambulizi ya kijeshi."


Kuanguka kwa Mobutu na Vita vya Kongo


Mwaka 1997, Makenga alikuwa sehemu ya vikosi vilivyoungwa mkono na Rwanda ambavyo vilimuondoa madarakani dikteta Mobutu Sese Seko na kumuweka mamlakani Laurent Kabila.


Hata hivyo, Makenga alianza kukosana na viongozi wake na kudai kuwa Kabila alikuwa anawatenga wapiganaji wa Kitutsi waliokuwa DRC.


"Kabila alikuwa mwanasiasa, lakini mimi siyo. Mimi ni askari, na lugha ninayojua ni ya bunduki," alisema Makenga.


Baada ya mzozo wa Kabila na Rwanda kuongezeka, serikali ya Kigali iliamua kuivamia tena DRC mwaka 1998, jambo lililozua Vita vya Pili vya Kongo, vilivyopelekea vifo vya zaidi ya watu milioni tano.


Katika kipindi hiki, Makenga aliteuliwa kuwa kamanda wa waasi walioungwa mkono na Rwanda na kuendelea kushiriki vita vilivyochochewa na rasilimali za madini za DRC.


Kuibuka kwa M23 na Uongozi wa Makenga

Baada ya miaka mingi ya mapambano, serikali ya DRC ilianzisha mpango wa kuwarejesha waasi wa Kitutsi jeshini, mpango uliokuwa ukijulikana kama mixage.


Hata hivyo, mwaka 2012, hali ilibadilika tena. Makenga alitoroka kutoka jeshi la serikali na kujiunga na kundi jipya la waasi – M23. Kundi hili lilisema linapigania haki za Kitutsi mashariki mwa DRC na kudai kuwa serikali ya Kinshasa imeshindwa kutekeleza makubaliano ya amani ya mwaka 2009.


Makenga alipanda cheo na kuwa kamanda wa M23, na mnamo Novemba 2012, aliongoza waasi hao kuteka jiji la Goma, jiji lenye watu zaidi ya milioni moja.

Umoja wa Mataifa na DRC waliilaumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi, tuhuma ambazo Kigali ilikanusha.

Mwaka huo huo, Marekani iliweka vikwazo kwa Makenga, ikisema kuwa anahusika katika "kuajiri watoto kama wanajeshi, na kampeni za ukatili dhidi ya raia."

Hata hivyo, Makenga alikanusha tuhuma hizi na kusema:

"Habari kwamba M23 inatumia watoto kama wanajeshi hazina msingi wowote."

Baada ya miezi michache ya utawala wa Goma, Umoja wa Mataifa ulituma kikosi maalum cha wanajeshi 3,000 kusaidia jeshi la DRC kurejesha jiji hilo. Makenga alilazimika kuondoka na kukimbilia Uganda.


Kurudi kwa M23 na Mgogoro wa Sasa

Kwa miaka mingi, Makenga alikuwa mafichoni. Lakini mwaka 2021, M23 ilirudi vitani na kuteka maeneo mbalimbali ya Kivu Kaskazini.


Juhudi za amani zimeshindwa mara kadhaa, na mwaka 2023, Mahakama ya DRC ilimhukumu Makenga adhabu ya kifo bila kuwepo mahakamani.


Hivi sasa, inaripotiwa kuwa M23 inapata msaada kutoka kwa wanajeshi wa Rwanda, jambo linaloongeza mvutano kati ya Kigali na Kinshasa.


Hata hivyo, tofauti na miaka ya nyuma, Makenga hajaonekana hadharani, badala yake amewakabidhi kazi hiyo msemaji wake na Corneille Nangaa, kiongozi wa muungano wa vikundi vya waasi.


Lakini kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa za Kongo, Makenga bado ana ushawishi mkubwa ndani ya M23 na anaendelea kupanga mikakati ya kijeshi.


Katika mahojiano ya awali, alieleza kuwa anaendesha vita kwa ajili ya familia yake:

"Ninapigana kwa ajili ya watoto wangu watatu, ili siku moja wawe na maisha bora katika nchi hii."


Lakini kwa mamilioni ya wakazi wa mashariki mwa DRC, mzozo huu umeleta maafa makubwa na kuwalazimu kuishi kama wakimbizi.


Iwapo Makenga atakamatwa na serikali ya Congo, adhabu yake tayari imeshaamuliwa – kifo.


Hata hivyo, kiongozi huyo wa M23 bado ana msimamo thabiti:

"Niko tayari kutoa kila kitu."

0 Comments:

Post a Comment