"Sina uchungu. Nina furaha sana," alisema Raila Odinga, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, baada ya kukubali matokeo ya uchaguzi wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), ambapo alishindwa na Mahamoud Ali Youssouf, Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti. Uchaguzi huo ulifanyika Jumamosi usiku huko Addis Ababa, Ethiopia.
Raila alikubali matokeo ya uchaguzi kwa kusema: “Ninakubali matokeo ya kura. Kwa hivyo mimi mwenyewe ninakubali kushindwa. Wanasema kwamba lazima tuimarishe demokrasia katika bara la Afrika na ninataka tutumie hii kama mfano mwema.”
Raila alisisitiza kuwa, licha ya kushindwa, aliwashukuru wale wote waliompigia kura na wale ambao hawakumpigia, akisema: "Nawashukuru watu wote waliompigia kura na wale ambao hawakumpigia, kwa sababu wametumia vyema haki zao za kidemokrasia."
Katika mazungumzo yake, Raila alieleza kuwa alikuwa tayari kwa matokeo yoyote, ama kushinda au kushindwa.
Alisema: "Sina machungu. Nina furaha sana na kama haitoshi, bado ninapatikana kutoa huduma yoyote kwa bara hili katika uwezo mwingine wowote."
Alielezea safari yake ya kampeni, akisema: "Nilijitolea kama mgombea, na kwa miezi kadhaa iliyopita nimetembea maeneo mbalimbali kukutana na viongozi, nikiwarai wanipigie kura. Leo wamejieleza na hali ilivyo, ni kwamba hatukufanikiwa."
Raila pia alizungumzia hali ya usawa barani Afrika, akisema: “Ninashukuru sana kwa zoezi la leo. Ninawashukuru watu wa Afrika.”
Alipoulizwa kuhusu hatua inayofuata baada ya kushindwa, Raila alijibu kwa kirefu, akisema: “Sasa nitarudi nyumbani, kuna mambo mengi ya kufanya.”
Pamoja na uchaguzi, Raila alizungumzia changamoto inayokabili Afrika, hasa mzozo wa kisiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Alisema: “Suala la DRC bado linaendelea kuwa tata. Mateso tunayoshuhudia hayakubaliki kabisa. Watu wasio kuwa na hatia wanauawa, watoto, wanawake na kadhalika. Lazima isitishwe.”
Kwa upande mwingine, Mahamoud Ali Youssouf, ambaye alishinda uchaguzi huo, alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 33 katika raundi ya saba, akimshinda Raila Odinga ambaye alijiondoa katika raundi ya sita.
Youssouf alikubali ushindi wake na alisema kwamba anajivunia kushinda uchaguzi huo na anatarajia kufanya kazi kwa bidii katika kuendeleza demokrasia na ushirikiano wa bara la Afrika.
Raila alikiri kwamba alikuwa na wakati mgumu katika mashindano haya, lakini aliunga mkono juhudi za demokrasia na ushirikiano wa kifedha, kisiasa na kijamii kati ya mataifa ya Afrika. "Tutatumia hii kama fursa ya kujifunza na kuendelea mbele kwa ajili ya mustakabali bora wa bara letu," alisema Raila.
Muhtasari wa Uchaguzi
Katika raundi ya kwanza ya uchaguzi, Raila Odinga alipata kura 20, Mahamoud Ali Youssouf alipata kura 18, na Richard Randriamandrato wa Madagascar alipata kura 10.
Nchi moja ilikosa kupiga kura. Katika raundi ya pili, Raila alipata kura 22, Youssouf alipata 19, huku Randriamandrato akipata kura 7.
Katika raundi ya tatu, Youssouf alichukua uongozi kwa kura 23, Raila akipata 20, na Randriamandrato akipata kura 5, huku nchi moja ikikosa kupiga kura.
Katika raundi ya nne, Youssouf alipata kura 25, Raila alipata kura 21, na kura moja ikaharibika. Waliokosa kupiga kura walikuwa mataifa mawili.
Katika raundi ya tano, Youssouf alipata kura 26, Raila alipata 21. Hakukuwa na kura zilizoharibika, lakini taifa moja lilikosa kupiga kura. Katika raundi ya sita, Youssouf alipata kura 26, Kenya ilipata kura 22, huku taifa moja likikosa kupiga kura.
Katika raundi ya saba, Mahamoud Ali Youssouf alipata kura 33 na alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa uenyekiti wa Tume ya AUC.
Raila Odinga amekubali matokeo ya uchaguzi, akitoa mfano mzuri wa kuvumilia na kukuza demokrasia barani Afrika. Ingawa alishindwa, alionesha utayari wa kuendelea kutoa mchango wake kwa bara hili katika nafasi yoyote ile.
Kwa upande mwingine, Mahamoud Ali Youssouf ameahidi kuendeleza juhudi za kuimarisha ushirikiano na demokrasia Afrika, huku akiongoza Tume ya AUC.

0 Comments:
Post a Comment