Serikali Yataka Mikoa Yote Kutumia Mfumo wa Ofisi ya Kielektroniki



Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, ameagiza mikoa ambayo bado haijaanza kutumia utaratibu wa Ofisi ya Kielektroniki (e-Office) kuhakikisha inaanza kutumia mfumo huo ifikapo tarehe 30 Juni mwaka huu. 

Aidha, ameagiza kituo cha utafiti kuimarishwa na kuongezewa eneo la ufanyaji kazi ili kuongeza ufanisi katika shughuli za Serikali Mtandao.






Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha Tano cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kinachofanyika jijini Arusha, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA na kada nyingine kwa kuweka mazingira wezeshi ya ufundishaji katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.



Amesisitiza kuwa taasisi zote za umma zinapaswa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao katika hatua zote za ujenzi au ununuzi, usimamizi na uendeshaji wa miradi ya TEHAMA.


"Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya ufundishaji katika vyuo vikuu na taasisi za serikali ili kuleta ukomavu katika utoaji wa huduma," amesema.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akipokea tuzo iliyotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Mhandisi Benedict Ndomba



Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, amesema kikao hicho kinawakutanisha wadau mbalimbali wa Serikali Mtandao kutoka taasisi na mashirika ya umma pamoja na sekta binafsi ili kujadili hatua iliyofikiwa na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa jitihada hizo.


"Tanzania imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za kidigitali ambapo ilishika nafasi ya pili barani Afrika kwenye Ripoti ya Utafiti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2022 kuhusu Ukomavu wa Matumizi ya Teknolojia Duniani katika utoaji wa huduma za serikali," amesema Simbachawene.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu,  Mululi Mahendeka, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda katika picha ya pamoja na wajumbe wa bodi ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).


Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba, amesema mamlaka hiyo imeiwezesha serikali kuwa na udhibiti wa moja kwa moja wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA inayotumika serikalini pamoja na kulinda usalama wa taarifa za serikali.




Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amesema Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu itaadhimishwa kwa wiki nzima, badala ya siku moja kama ilivyozoeleka.



"Sherehe ya Siku ya Wanawake Kitaifa Arusha tunafanya kitu cha tofauti. Hatutafanya tu tarehe 8 Machi, bali tumeamua kuanza tarehe 1 Machi kwa wiki nzima ya shughuli mbalimbali za kuwawezesha wanawake," amesema Makonda.


Ameeleza kuwa shughuli hizo zitahusisha utoaji wa huduma za afya, msaada wa kisheria, elimu ya fedha na michezo kama mpira wa miguu kwa wachezaji wa kike kutoka timu za Simba Queens, Yanga Queens, JKT Queens na Fountain Gate FC.



Kikao Kazi cha Tano cha Serikali Mtandao kimehudhuriwa na zaidi ya washiriki 1,300 kutoka taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi. 


Kauli mbiu ya kikao hicho ni "Jitihada na Ubunifu wa Serikali Mtandao kwa Utoaji wa Huduma za Umma kwa Ufanisi."

0 Comments:

Post a Comment