Suala la upotevu wa zaidi ya shilingi milioni 400 za Umoja wa Bodaboda Mkoa wa Arusha limechukua sura mpya baada ya viongozi wa umoja huo kuiomba serikali iingilie kati ili fedha hizo zipatikane na kusaidia kukuza uchumi wa vijana hao.
Katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika Alhamisi, Februari 27, 2025, viongozi wa bodaboda waliibua malalamiko hayo na kueleza kuwa fedha hizo, zilizochangwa na wadau mbalimbali mwaka 2018, zilianza kuchotwa kupitia matawi mbalimbali ya benki kuanzia mwaka 2020.
Kutokana na malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ameipa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) muda wa mwezi mmoja hadi Machi 27, 2025, kuhakikisha uchunguzi unakamilika na ripoti inatolewa kwa wanahabari.
Malalamiko ya Viongozi wa Bodaboda
Katibu wa Umoja wa Bodaboda Mkoa wa Arusha, Hakim Msemo, amesema kuwa juhudi zao za kufuatilia suala hilo hazijazaa matunda licha ya kuwa na taarifa za baadhi ya waliotuhumiwa.
"Mimi nimeenda hadi Dar es Salaam, kufuatilia na nikapata hata namba ya gari la mwenyekiti, ila Takukuru hawakumfuata wala kuchukua hatua. Tumeenda nyumbani kwa mwingine Sinoni, tulipopeleka taarifa Takukuru hawakuchukua hatua," amesema.
Ameongeza kuwa walipata taarifa za mmoja wa watia saini wa akaunti hiyo kuwa ametokea Dar es Salaam na kuelekea Rombo kutibiwa, lakini hata baada ya kuwataarifu Takukuru, hatua hazikuchukuliwa.
Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo, Hemed Mbaraka, ameonya kuwa wanasiasa wanapaswa kutoingilia masuala ya bodaboda kwa maslahi yao binafsi.
"Yeyote atakayetuingilia na kutaka kutugawa kwa maslahi ya kisiasa tutamfikisha kwa uongozi wa mkoa," amesema.
Hatua za Uchunguzi
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amesema kuwa suala hilo linapaswa kufika mwisho na wahusika wote wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
"Kama hawa bodaboda wanajua mahali wahalifu walipo, inakuaje nyie mamlaka ya uchunguzi mnashindwa kuwapata? Takukuru, unajisikiaje kuwa na jalada lisilofikia mwisho?" amehoji.
Ameongeza kuwa kama hadi Machi 27, 2025 ripoti ya uchunguzi haitakuwa imetolewa, basi itahitimishwa kuwa baadhi ya maafisa wa Takukuru ni sehemu ya wanufaika wa upotevu wa fedha hizo.
"Suala hili limesemwa sana hadi limekuwa kero, nawapa muda hadi Machi 27, 2025, mtoe ripoti mmefikia wapi kwenye uchunguzi wa suala hili. Tukikosa majibu, tutahitimisha kuwa Takukuru ni sehemu ya wanufaika," amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Daniel Kapakala, amesema kuwa uchunguzi wa suala hilo umeshafanyika, lakini tatizo kubwa limekuwa ni kuwapata watuhumiwa waliotoroka.
"Watu wa benki nao tumeshawahoji, mbunge pia na watu wengine, ila kilichobaki ni kuwapata hao watu na tumeanza kuwatafuta tangu mwaka 2023," amesema.
Ameongeza kuwa akaunti ya akina mama waliokopeshwa shilingi milioni 120 imeshafungwa na mpaka sasa shilingi milioni 68 zimerejeshwa.
Sakata hili limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu, ambapo Desemba mwaka jana, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa (UVCCM), Mohamed Kawaida, alisema kuwa suala hilo litafikishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan ili fedha hizo zirejeshwe kwa wahusika.
Kikao hicho cha RCC pia kiliidhinisha bajeti ya Mkoa wa Arusha ya shilingi bilioni 430.7 kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026.







0 Comments:
Post a Comment