Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umetangaza kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Walimu wasio na Ajira Tanzania (NETO), Mwalimu Joseph Paulo Kaheza, ambaye alikuwa akishikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Geita, amepewa dhamana.
Katika taarifa yake, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo ole Ngurumwa, ameeleza kuwa pamoja na kuachiwa, Jeshi la Polisi limeendelea kushikilia simu mbili za Mwalimu Kaheza.
"Baada ya kuachiwa kwa dhamana, Polisi wamemuahidi kwamba simu zake arudi kuzichukua kesho Februari 26, 2025," amesema ole Ngurumwa.
Kwa mujibu wa THRDC, wakati akiwa mikononi mwa Polisi, Mwalimu Kaheza alihojiwa kuhusu Umoja wa Walimu wasio na Ajira Tanzania (NETO) pamoja na makundi ya WhatsApp yanayojulikana kwa jina la NETO.
Ufuatiliaji wa Dhamana
Wakili ole Ngurumwa amesema kuwa asubuhi ya Februari 25, 2025, THRDC iliwaagiza mawakili wawili, Wakili Benard Otieno na Wakili Vianey Mbuya, kufuatilia dhamana ya Mwalimu Kaheza katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Geita.
"Baada ya mawakili hao kufika kituo cha Polisi mjini Geita hawakumkuta Mwalimu Kaheza, badala yake waliambiwa waende kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Geita ambaye ndiye alikuwa anamshikilia," amesema ole Ngurumwa.
Kwa sasa, Mwalimu Kaheza anatakiwa kuripoti tena katika Kituo Kikuu cha Polisi Geita mnamo Februari 27, 2025.
Chanzo cha Kukamatwa
Kukamatwa kwa Mwalimu Kaheza kunakuja siku chache baada ya kutoa malalamiko kuhusu mamia ya walimu waliokuwa wakijitolea kufundisha kutopata ajira za kudumu zilizotangazwa na serikali.
Katika malalamiko hayo, aliitaka serikali kuhakikisha walimu hao wanapewa ajira rasmi.
THRDC imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia suala hili kwa karibu ili kuhakikisha kuwa Mwalimu Kaheza anapata haki zake kwa mujibu wa sheria.
0 Comments:
Post a Comment