Kampeni ya "MTU NI AFYA" Yafika Jijini Arusha

 

Leo, Balozi wa Kampeni ya "MTU NI AFYA," Mrisho Mpoto maarufu kama Mjomba, alifanya ziara rasmi Jijini Arusha kwa lengo la kusaini hati ya makubaliano ya utekelezaji wa kampeni hiyo inayoratibiwa na Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais-Tamisemi. 





Alipokelewa na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John L. Kayombo, ambaye alionyesha kuunga mkono juhudi hizo zinazolenga kuboresha afya ya jamii.

Kampeni ya "Mtu ni Afya," ilizinduliwa rasmi na Makamu wa Rais, Philip Mpango, tarehe 09 Mei 2024, na inajikita katika maeneo muhimu ya afya ya jamii. 


Imejumuisha hatua tisa muhimu, ambazo ni: ujenzi wa vyoo bora na kuvitumia, unawaji mikono katika nyakati maalum, usafi maeneo ya kazi na makazi, udhibiti wa utupaji taka hovyo, mazoezi ya mwili, hedhi salama, lishe bora, uandaji wa maji safi na salama, na matumizi ya nishati safi ya kupikia.




Akizungumza kuhusu kampeni hiyo,  Mpoto alieleza kuwa, "Lengo kuu la kampeni ya Mtu ni Afya ni kujikita zaidi katika huduma za kinga badala ya kwenye tiba." Alisema kuwa lengo ni kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuzingatia afya yao mapema ili kuepuka magonjwa na athari za kiafya zinazoweza kuepukika.



Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo, alionesha furaha na kuridhika na ujio wa kampeni hiyo, akisema, "Kampeni hii imekuja wakati muafaka Jijini Arusha, na tutahakikisha tunatoa ushirikiano wa hali na mali ili kufanikisha malengo yake." 


Aliongeza kuwa Arusha, ikiwa ni mkoa wa tisa katika utekelezaji wa kampeni hii, itafaidika sana kwa kubadilisha fikra za jamii kuhusu afya na usafi.


Kampeni hii imefanyika katika mikoa nane tofauti hapa nchini, na sasa mkoa wa Arusha unapata fursa ya kuwa sehemu ya harakati hizi. 


Mikutano mitatu ya hadhara itafanyika Jijini Arusha ili kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kubadilisha tabia za kiafya, ikiwa ni pamoja na kuzingatia usafi na afya bora.



Kwa kumalizia, Mrisho Mpoto alitoa shukrani kwa uongozi wa Jiji la Arusha kwa mapokezi mazuri na alisisitiza kuwa, "Tutafanya kazi kwa karibu na viongozi wa mkoa huu ili kufikia malengo ya kampeni hii kwa manufaa ya afya ya wananchi wa Arusha na taifa kwa ujumla."

0 Comments:

Post a Comment