INEC Kuanza Mchakato wa Kugawa na Kubadili Majina ya Majimbo ya Uchaguzi



Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuanza mchakato wa kuchunguza, kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi ambapo itapokea mapendekezo kuanzia tarehe 27 Februari, 2025 hadi tarehe 26 Machi, 2025.


Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele, amesema hayo leo tarehe 26 Februari, 2025 muda mfupi baada ya kumaliza kuongoza kikao cha Tume kilichofanyika mkoani Morogoro.


"Kwa kuzingatia masharti ya Kanuni ya 18(1) ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za mwaka 2024, napenda kutoa taarifa kwa umma kwamba, kuanzia kesho siku ya Alhamis tarehe 27 Februari, 2025, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi itaanza mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi," amesema Jaji Mwambegele.


Akifafanua kuhusu muda wa kupokea maombi, Jaji Mwambegele amesema, "Maombi yote ya kugawa au kubadilisha jina la jimbo yawasilishwe Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuanzia tarehe 27 Februari, 2025 hadi tarehe 26 Machi, 2025."


Ameeleza kuwa Tume inatekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa Ibara ya 74(6)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Kifungu cha 10(1)(d) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024, kinachotoa mamlaka kwa Tume kuchunguza mipaka na kuigawa nchi katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa Wabunge.


"Kwa mujibu wa Ibara ya 75(4) ya Katiba, jukumu hilo linaweza kufanywa mara kwa mara na angalau kila baada ya miaka kumi. Kwa mara ya mwisho, Tume ilichunguza mipaka na kugawa majimbo ya uchaguzi mwaka 2015, ambapo majimbo mapya 26 yalianzishwa," amesema Jaji Mwambegele.


Ameeleza kuwa wadau wote wenye maombi wanapaswa kuhakikisha mapendekezo yanajadiliwa katika Kamati ya Ushauri ya Wilaya kabla ya kuwasilishwa kwa Katibu Tawala wa Mkoa kwa ajili ya kujadiliwa katika Kamati ya Ushauri ya Mkoa. Mapendekezo yaliyopitishwa katika kikao hicho yatawasilishwa Tume pamoja na viambatisho vyote husika.


Amesema vigezo vya kugawa au kubadili majina ya majimbo ni wastani wa idadi ya watu, ambapo majimbo ya mijini yanapaswa kuwa na watu 600,000 na ya vijijini watu 400,000.


"Idadi ya watu itakayotumika ni ile iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022," amesema.


Vigezo vingine vitakavyozingatiwa ni hali ya kiuchumi ya jimbo, ukubwa wa eneo lake, mipaka ya kiutawala, mpangilio wa makazi ya watu, uwezo wa ukumbi wa Bunge, idadi ya Wabunge wa Viti Maalum Wanawake, upatikanaji wa njia za mawasiliano na hali ya kijiografia ya eneo husika.


"Halmashauri zinazokusudia kubadili jina la jimbo zinapaswa kufuata utaratibu sawa na ule wa kuwasilisha maombi ya kugawa majimbo," amesema Jaji Mwambegele.

0 Comments:

Post a Comment