Entebbe, Uganda – Wanafamilia wanne wa kiongozi wa waasi wa Uganda, Joseph Kony, ambaye anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa uhalifu wa kivita, wamehamishwa na kurejeshwa nchini Uganda baada ya kuishi kwa miaka mingi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) chini ya kundi la waasi la Jeshi la Upinzani la Bwana (LRA).
Watu hao ni mke wa zamani wa Kony, mabinti wawili, na mvulana mmoja, ambao walitoroka kutoka kambi ya LRA mwaka jana. Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor, walisaidiwa kurejea nchini na shirika la kimataifa la PAX-Netherlands, ambalo limekuwa likihusika katika juhudi za kuwarejesha waasi wa zamani wa LRA na familia zao.
Walipowasili usiku katika Uwanja wa Ndege wa Entebbe, Waziri wa Nchi wa Uganda anayehusika na Kanda ya Kaskazini, Kenneth Omona, aliwasihi waasi wengine wa LRA waliobaki msituni wajisalimishe kwa serikali ya Uganda.
"Tunaendelea kuwasihi waliobaki msituni warudi nyumbani. Mlango bado upo wazi, na wote waliojisalimisha wamepewa msamaha, kama vile wale waliorejea leo," alisema Waziri Omona.
Waziri huyo alieleza kuwa marais wa Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Yoweri Museveni na Faustin Archange Touadéra, walifanya mazungumzo maalum ili kuwezesha kurejeshwa kwa wanachama hao wa familia ya Kony.
Kwa zaidi ya miaka 20, LRA ya Joseph Kony imetuhumiwa kutekeleza uhalifu wa kivita ikiwemo mauaji, ubakaji, na utekaji wa watoto ili kuwafanya askari wa waasi katika Kaskazini mwa Uganda. Kundi hilo lilidai kupigania kuanzisha utawala unaozingatia Amri Kumi za Biblia, lakini lilihusika katika ghasia kubwa dhidi ya raia.
Mnamo mwaka 2006, Jeshi la Uganda (UPDF) lililazimisha kundi hilo kuondoka Uganda, na tangu wakati huo, waasi wake wamekuwa wakijificha katika misitu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mwaka jana, Mahakama ya Uganda ilimhukumu Thomas Kwoyelo, mmoja wa makamanda wa zamani wa LRA, kifungo cha miaka 40 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya makosa 44 yakiwemo mauaji, ubakaji, na utekaji nyara. Hata hivyo, Kwoyelo alikana mashitaka hayo.
Mpaka sasa, Joseph Kony bado anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na inadhaniwa kuwa anaendelea kujificha katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
0 Comments:
Post a Comment