Waziri Jafo Aagiza Mabadiliko CAMARTEC Katika Uzalishaji na Usimamizi wa Zana za Kilimo

 


Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) kufanya mabadiliko makubwa katika uzalishaji na udhibiti wa zana za kilimo, huku akisisitiza matumizi sahihi ya fedha na kuhakikisha taasisi hiyo haipati hati chafu. 



Dkt. Jafo alitoa maelekezo hayo Januari 24, 2025, wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya CAMARTEC jijini Arusha.


Waziri Jafo alisisitiza kuwa Bodi hiyo inapaswa kuhakikisha zana za kilimo zinawafikia wananchi wengi, hasa wakulima, na kuendelea kutoa ushauri ili kuboresha ubunifu na maendeleo ya taasisi hiyo. Aliongeza kuwa CAMARTEC inatakiwa kuwa na mabadiliko makubwa ili kuendana na teknolojia ya kisasa na kusaidia sekta ya kilimo kupata tija.


Vilevile, alizitaka Taasisi zote chini ya Wizara yake kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya Kitengo cha Habari na Mawasiliano ili kutejeleza majukumu yake katika kuelimisha umma kuhusu maendeleo ya sekta ya viwanda na biashara.


Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Needpeace Wambuya, alieleza kuwa Bodi hiyo itahakikisha tafiti na majaribio ya teknolojia yanahusishwa na zana za kilimo kutoka nje ya nchi.


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CAMARTEC, Injinia Godfrey Mwinama, alifafanua kuwa Kituo hicho kimefanikiwa kuunda zana mpya 42 zinazozalisha zana mbalimbali zinazolenga kuongeza tija katika kilimo.


Mwenyekiti wa Bodi ya CAMARTEC, Profesa Valerian Silayo, alithibitisha kupokea maelekezo yote na kusema Bodi iko tayari kutekeleza majukumu hayo kwa kuhakikisha CAMARTEC inafikia malengo yake.

0 Comments:

Post a Comment