Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Nishati (Africa Energy Summit) utakaofanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 27 - 28 Januari, 2025.
Mkutano huu unaandaliwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia, na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Marais wa Nchi 24 za Afrika, wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika 21, Wakuu wa Taasisi za Kimataifa sita, wakiwemo Rais wa Benki ya Dunia, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na Rais wa Taasisi ya Rockefeller, watashiriki katika mkutano huu.
Aidha, jumla ya washiriki 2,600 kutoka ndani na nje ya Tanzania wamejisajili kushiriki katika mkutano huu.
Kufuatia ugeni huu mkubwa, baadhi ya barabara muhimu za Jiji la Dar es Salaam zitafungwa kama ilivyotangazwa na Jeshi la Polisi.
Hivyo, ili kuepuka usumbufu ambao unaweza kusababishwa na kufungwa kwa barabara hizo, Serikali imeelekeza kuwa tarehe 27 na 28 Januari, 2025, watumishi wa umma katika Mkoa wa Dar es Salaam wafanyie kazi nyumbani, isipokuwa wale ambao mazingira yao ya kazi yanawataka kuwepo katika vituo vya kazi kama vile watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, sekta ya afya na sekta ya usafiri na usafirishaji.
"Hivyo, Benki hazitafungwa na biashara katika Soko la Kariakoo zitaendelea kufanyika.
Hoteli na migahawa nayo haitafungwa," ilieleza sehemu ya taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi.
Aidha, waajiri katika sekta binafsi wanashauriwa kuruhusu watumishi wao katika Mkoa wa Dar es Salaam kufanyia kazi nyumbani au kuweka utaratibu ambao hautasababisha changamoto ya usafiri kutokana na kufungwa kwa barabara hizo.

0 Comments:
Post a Comment