Jeshi la Polisi mkoa wa Morogoro limefanikiwa ya kumpata mtoto Shamimu Nasibu Ndihagule (2) ambaye alielezwa kuwa ameibiwa kutoka kwa wazazi wake, katika tukio lililotokea Januari 15, 2025 asubuhi katika kitongoji cha Kisiwani, kijiji cha Tundu, kata ya Kidodi, wilaya ya kipolisi Ruhembe.
Mtoto huyo alichukuliwa na mtu asiyefahamika wakati akicheza na mtoto mwenzake, Josephat Natalis Jangama (3), mkazi wa kitongoji hicho.
Mtoto Shamimu alipatikana akiwa salama katika eneo la kitongoji cha Mhovu, kijiji cha Kisinga, kata ya Ruaha, wilaya ya kipolisi Ruhembe, Januari 19, 2025 asubuhi, kwenye mashamba ya miwa, baada ya kufuatiliwa na jeshi la polisi ambao walikuwa wakitekeleza msako mkali.
Mtoto huyo kwa sasa anapatiwa matibabu na vipimo katika Kituo cha Afya Kidodi ili kuhakikisha afya yake inakuwa salama.
Jeshi la polisi limekamata mtuhumiwa mmoja, ambaye ni mganga wa tiba za asili, kama sehemu ya uchunguzi wa tukio hili. Jina la mtuhumiwa linahifadhiwa kwa sasa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amewashukuru wananchi wote waliojitolea kwa ushirikiano wao katika kumtafuta mtoto Shamimu.
Aidha, amewataka wazazi kuongeza ulinzi kwa watoto wao ili kuepuka matukio kama haya ambayo yanaweza kuleta taharuki katika jamii.

0 Comments:
Post a Comment