MAREKANI YASITISHA MISAADA YA KIGENI ISIPOKUWA KWA ISRAELI NA MISRI

 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesitisha karibu misaada yote ya kigeni iliyokuwa ikiendelea na kuzuia utoaji wa misaada mipya. 



Hatua hii inafuatia agizo kuu la Rais Donald Trump alilolitoa siku ya Jumatatu, likitaka kusitishwa kwa muda wa siku 90 kwa misaada ya maendeleo ya kigeni, ili kufanyiwa mapitio ya ufanisi na uthabiti wa sera za Marekani katika uwanja wa kimataifa.


Taarifa ya ndani iliyotumwa kwa maafisa wa wizara hiyo na balozi za Marekani nje ya nchi imebainisha kuwa misaada itakayositishwa ni pamoja na usaidizi wa maendeleo na usaidizi wa kijeshi, isipokuwa misaada ya dharura ya chakula pamoja na ufadhili wa kijeshi kwa Israeli na Misri.


“Fedha za Marekani zinapaswa kutumika nje ya nchi tu pale ambapo zinaiweka Marekani kuwa nchi yenye nguvu, salama, au yenye kustawi zaidi,” alisema Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, akieleza msingi wa maamuzi haya.


Marekani, ambayo ndiyo mfadhili mkubwa zaidi wa misaada ya kigeni duniani, ilitumia dola bilioni 68 katika mwaka wa 2023 kwa ajili ya misaada hiyo, kulingana na takwimu za serikali.


Hatua hiyo imeibua maswali na mjadala mpana katika jumuiya za kimataifa, huku mashirika ya habari ya kimataifa, ikiwemo BBC, yakithibitisha maudhui ya taarifa hiyo iliyovuja.

0 Comments:

Post a Comment