Halmashauri ya Jiji la Arusha leo Januari 28, 2025, imezindua mitambo maalum yenye thamani ya shilingi bilioni 1.7, ikiwa ni hatua muhimu ya kumaliza changamoto ya barabara mbovu katika maeneo mengi ya jiji hili.
Mitambo hii itahusika na ukarabati wa barabara zinazohusiana na Jiji, ambazo haziko chini ya usimamizi wa TARURA.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo, alisisitiza kuwa ununuzi wa mitambo hiyo ni matokeo ya juhudi za halmashauri kuhakikisha barabara za mitaa zinafanyiwa marekebisho kwa ufanisi, na kumaliza changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara.
“Mitambo hii tumenunua kwa fedha zetu za ndani, hivyo ni jukumu la kila mkazi wa Arusha kujivunia uwepo wa mitambo hii. Napenda kutoa rai kwa kila mwana Arusha kuwa mlinzi wa mitambo hii,” alisema Kayombo.
Kayombo alieleza kwamba mitambo hiyo inajumuisha greda moja la kuchonga barabara na malori makubwa mawili, na inatarajiwa kugusa mitaa 154 katika kata 25 za jiji hilo.
“Halmashauri yetu iliweza kutenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ununuzi wa mitambo na malori, ila kwa neema ya Mungu tumeweza kununua nyenzo hizi kwa thamani ya shilingi bilioni 1.7 na fedha zilizobaki zitagawanywa kwa kila kata kiasi cha shilingi milioni 4 kwa ajili ya ununuzi wa vifusi,” alisema Kayombo.
Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iraghe, alishukuru halmashauri kwa hatua hiyo na kuwataka madiwani kutekeleza jukumu lao kwa kuhakikisha barabara zinazotambuliwa kama mbovu katika kata zao zinapata kipaumbele.
“Niwaombe madiwani wenzangu twenda kuainisha maeneo korofi kwenye kata zetu ili barabara zetu ziweze kutengenezwa na kuondokana na changamoto za miundombinu ya barabara kwa wananchi ili waweze kufurahia serikali yao,” alisema Iraghe.
Mitambo hii imekuja baada ya hali mbaya ya barabara kusababisha hali ya usumbufu kwa wananchi, ambapo baadhi ya madiwani walikumbwa na aibu ya kutembezwa kwenye madimbwi ya maji kwa kushinikiza ujenzi wa barabara.
Diwani wa kata ya Murieti, Francis Mbise, alikumbwa na tukio hilo mwishoni mwa mwaka 2024, ambapo wananchi walimkamata pamoja na viongozi wengine na kuwatembeza kwenye maeneo yenye mivujio ya maji ili kuonyesha hasira zao kutokana na barabara mbovu.
Hata hivyo, uzinduzi wa mitambo hii unaonekana kuwa ni suluhisho la kudumu kwa changamoto ya barabara za jiji la Arusha, hasa ikizingatiwa kwamba barabara nyingi za mitaani hazikupata kipaumbele kutoka kwa TARURA, kutokana na upana wake kuwa chini ya mita 12. Hii inafanya kazi ya ukarabati kuwa vigumu.
Madiwani wa jiji hilo, wakiwemo Saluni Olodi (Sokoni One), Karimu Mushi (Engutoto), na Francis Mbise (Murieti), walishukuru halmashauri kwa uamuzi huo na kueleza jinsi ununuzi wa mitambo hiyo utakavyosaidia kutatua changamoto ya barabara, ambayo iliwalazimu kuonyeshwa dhihaka na wananchi kwa kutembezwa kwenye madimbwi ya maji.
Karimu Mushi, Diwani wa kata ya Engutoto, alisema, “Nashukuru halmashauri kwa kusikia kilio cha wananchi na kutenga fedha hizi kwa ajili ya kununua mitambo hii.”
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Willfred Soilel Mollel, alisisitiza umuhimu wa kutunza mitambo hii na kuhakikisha inatumika kwa lengo lililokusudiwa.
“Mitambo hii itasaidia kuwapunguzia kero wananchi hasa barabara ambazo hazipo kwenye mpango wa TARURA,” alisema Mollel, akiagiza kwamba mitambo hiyo itunzwe ipasavyo ili kuepuka matumizi mabaya.
Kwa jumla, uzinduzi wa mitambo hii unaashiria hatua muhimu katika kuboresha miundombinu ya barabara za jiji la Arusha, na kuongeza matumaini ya kuondokana na changamoto zinazowakabili wananchi wengi wa jiji hili.











0 Comments:
Post a Comment