Godbless Lema, Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini na Mwenyekiti Mstaafu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, ametangaza rasmi kumunga mkono Tundu Lissu na John Heche katika kinyang’anyiro cha Uenyekiti wa chama hicho.
Lema amesema kuwa amefanya uamuzi huo kutokana na hali ya sasa ya chama na kudai kuwa chama kinahitaji mabadiliko ya kiuongozi.
Akizungumza na wanahabari, Lema alisema, "Nimeona kwenye maswali katika mitandao ya kijamii nikuliulizwa kwamba wewe unamuunga nani mkono? Wengine wanasema Lema toa msimamo.
Sasa leo nimekuja kutoa msimamo na mwelekeo wangu, namuunga mkono Tundu Lissu na John Heche."
Lema pia aliongeza kuwa Mbowe alimuambia mara kadhaa kwamba hatagombea tena uenyekiti lakini sasa ameonekana kugombea tena, jambo ambalo linawapa wasiwasi baadhi ya wanachama.
"Mbowe alimuambia zaidi ya mara 5 kuwa hataendelea na Uenyekiti lakini hatimaye anagombea tena," alisema Lema.
Aidha, Lema alieleza kuwa chama hakina budi kuangalia viongozi wanaoweza kuendesha chama na kulinda demokrasia ndani yake.
"Ikifika mahali kama mtu hana pesa hawezi kuwa kiongozi wa chama hiki, hiyo ni hatari kubwa, hata huyo anayetajwa ana pesa, ana pesa za kuendesha chama?" aliongeza Lema.
Lema alieleza kuwa anajivunia kuwaunga mkono Lissu na Heche kwa kuwa wanapigania ukweli na masuala muhimu kwa taifa.
"Lissu siyo mropokaji, kazi yetu kama wapinzani ni kupiga kelele kwenye masuala ya msingi, kwahiyo Lissu anapiga kelele kwenye masuala ya msingi," alisema Lema akikemea shutuma zinazotolewa dhidi ya Lissu.
Lema pia alitangaza kuwa kama Freeman Mbowe hataki kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha Uenyekiti, basi atachukua msimamo madhubuti.
"Ushauri wangu kwa Mwenyekiti ni kuwa ajiondoe kwenye huu Uchaguzi, amuunge mkono Lissu. Akipigwa chini kwenye Uchaguzi atakuwa ameiaharibu vibaya sana Legacy yake," alisisitiza Lema.
Mbali na msimamo wa kumunga mkono Lissu, Lema pia alitangaza kwamba hatawania tena kiti cha Ubunge wa Arusha Mjini mwaka 2025 ikiwa Mbowe atashinda uchaguzi wa Uenyekiti wa Chadema.
"Ninatangaza rasmi kuwa sitagombea Ubunge wa Arusha Mjini 2025 kama Mbowe atashinda uchaguzi wa Uenyekiti," alisisitiza.
Lema alieleza kuwa chaguo lake ni kwa ajili ya demokrasia na mabadiliko katika chama hicho.
"Sifanyi kazi ya uanaharakati kwa lengo la kuwa kiongozi, bali nafanya kazi ya uanaharakati kwa lengo la kutaka future ya wajukuu ili waje kuwa na maisha mazuri," alisema Lema, akionyesha wazi kuwa anapigania maslahi ya chama na taifa kwa ujumla.
Alimalizia kwa kusema, "Kaka yangu Mbowe kama hatutasalimiana tena sababu ya Msimamo wangu wa Kumuunga mkono Lissu, haina shida maisha yataendelea ila nitaumia sana."
0 Comments:
Post a Comment