Zoezi la Uokoaji Kariakoo Kuendelea kwa Saa 24 za Ziada kwa Agizo la Rais

SERIKALI imetangaza kuwa zoezi la uokoaji wa watu walionasa kwenye jengo lililoporomoka Jumamosi ya Novemba 16, 2024, katika Mtaa wa Congo na Mchikichi, Kariakoo Jijini Dar es Salaam, litaendelea kwa saa 24 za ziada. 



Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba, ametoa msimamo huo wa serikali leo Novemba 19 2024 wakati akiongea na waandishi wa habari kwenye eneo la tukio.


Hii ni baada ya saa 72 za kawaida za kimataifa kumalizika, kwa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.  



“Moja ya ajenda iliyozungumzwa kwenye kikao cha tathmini cha kazi inayoendelea ni kuhusiana na utaratibu wa uokoaji. 


Kulianza kutokea maneno kwenye mitandao ya kijamii kwamba baada ya masaa 72 kwa kawaida kwa viwango vya kimataifa, zoezi la uokoaji kwenye maeneo kama haya linabadilika, na wanaanza kutumia mashine pale inapolazimu.  


"Rais Samia Suluhu Hassan muda huu ametoa maelekezo kupitia kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, na maelekezo hayo yaje kwa kikosi chetu cha Zimamoto na Uokoaji kwamba zoezi hili liendelee kwa saa zingine 24 za ziada, ni kwamba wasisitishe, kabla ya kubadili hatua yoyote. 


Kwa hiyo, zoezi hili linaendelea, halitasitishwa kama ambavyo wananchi wengine wameanza kuwa na hofu.”  


Makoba aliongeza kuwa lengo la kuongeza muda huo ni kuhakikisha usalama wa watu walioko kwenye kifusi.  


“Imempendeza Rais Samia Suluhu Hassan kwamba tutaendelea kutumia mbinu ambazo zilikuwa zikitumika za weledi na ustadi zaidi katika kuhakikisha kwamba, kwanza tunaridhika kwamba hakuna ambaye aliyepo hai atasumbuliwa au ataangushiwa kifusi huko chini, au kwa namna yoyote ile itamkuta ili kumsababishia kupoteza maisha. Baada ya masaa 24 tutatangaza utaratibu unaofuata.”  


Zoezi hilo la uokoaji linaingia siku ya nne sasa, huku Serikali ikifanya jitihada kubwa kuhakikisha hakuna madhara yatakayowapata watu walionaswa kwenye jengo hilo.  

0 Comments:

Post a Comment