Viongozi wa Dini, Siasa na Mila Watoa Wito Kuhamasisha Uboreshaji wa Taarifa Kwenye Daftari la Wapiga Kura

 



Viongozi wa dini, wanasiasa, na viongozi wa mila wamehimiza ushirikiano wa pamoja katika kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu kwenye uboreshaji wa taarifa zao muhimu katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kama inavyotakiwa na sheria.  



Akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 30, 2024, jijini Arusha, Sheikh Haruna Hussein, Msemaji wa Taasisi ya Kiislamu ya Twariqa Qadiriya Razikia Jailania Tanzania, alitoa wito kwa wananchi na viongozi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo.  


"Ninawapongeza Tume ya Uchaguzi kwa juhudi zao za kuanza kutoa elimu kwa makundi maalum. Jana tumeona viongozi wa dini, wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, wahariri, waandishi wa habari, na viongozi wa mila wakielimishwa kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. 


Hii ni hatua muhimu kwa kuwa viongozi hawa watasaidia kufikisha ujumbe kwa watu wanaowaongoza," alisema Sheikh Haruna.  



Alisisitiza umuhimu wa wananchi kuhakiki taarifa zao, hususan wale waliohama kutoka maeneo yao au wanaotarajia kutimiza miaka 18 mwakani.  


"Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 74(6), Tume ya Uchaguzi imepewa mamlaka ya kuratibu uandikishaji wa wapiga kura. Ni muhimu kila mmoja wetu kushiriki katika zoezi hili ili kufanikisha uchaguzi bora mwaka 2025," aliongeza.  


Sheikh Haruna aliitaka Tume ya Uchaguzi kuhakikisha elimu hiyo inafika vijijini na kwa makundi maalum kama wajawazito, wanawake wenye watoto wachanga, na walemavu.  


"Kauli mbiu ya mwaka huu, 'Kujiandikisha kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora,' ni muhimu kuitekeleza kwa vitendo. Tunatoa wito kwa viongozi wa dini, mila, na vyama vya siasa kuhamasisha wafuasi wao kushiriki kikamilifu," alisema.  



Aliipongeza Tume kwa kuongeza vituo vya uandikishaji katika Wilaya ya Ngorongoro, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza umbali wa kutembea kwa wananchi na kurahisisha zoezi hilo.

  

"Kuongeza vituo vya uandikishaji ni hatua muhimu. Tunawasihi vijana wa miaka 17, ambao watatimiza miaka

 18 mwakani, kuhakikisha wanajiandikisha mapema. Zoezi hili ni msingi wa kushiriki uchaguzi," alisema Sheikh Haruna.  



Mchungaji Yohane Parkipumi wa Kanisa la Moraviani alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kudumisha amani na kutoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa.  


"Tunamshukuru Rais Samia kwa juhudi zake za kulinda na kuimarisha amani. Ninawaomba wachungaji, masheikh, na viongozi wa mila kuendelea kuliombea taifa hasa tunapoelekea uchaguzi mkuu mwaka ujao," alisema Mchungaji Parkipumi.  



Kwa upande wake, Sheikh Iddy Ngella alihimiza wananchi kutumia fursa ya amani iliyopo kukuza uchumi wa taifa. 

 

"Mahusiano mazuri kati ya Tanzania na majirani zake yanayojengwa na viongozi wetu ni fursa ya kukuza uchumi. Wananchi wa Arusha na Tanzania kwa ujumla, tumieni amani hii kuboresha maisha yenu na ya taifa," alisema Sheikh Ngella.  


Wananchi wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, na Dodoma wanatarajiwa kushiriki kwenye zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuanzia Desemba 11 hadi 17, 2024. 


Viongozi wamewataka wananchi wote kuhakikisha wanahakiki na kuboresha taarifa zao kwa wakati ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

0 Comments:

Post a Comment