Tukio la Utekaji la Tarimo: Polisi Waanza Uchunguzi, Wananchi Wakemea Matukio ya Utekaji



Jeshi la Polisi nchini Tanzania linachunguza tukio la utekaji lililojitokeza kwenye mitandao ya kijamii, likionesha juhudi za watu kumkamata kwa nguvu Deogratius Tarimo, mfanyabiashara na mkazi wa Kibaha, Mkoa wa Pwani. 



Katika tukio hilo, watekaji wanamjaribu kumwingiza kwa nguvu kwenye gari, huku mhanga akijitahidi kupigania uhai wake. 


Tukio hili liliripotiwa na mwenyewe, Deogratius Tarimo, katika Kituo cha Polisi cha Gogoni, Jijini Dar es Salaam, mnamo Novemba 11, 2024.


Chanzo cha Tukio



Taarifa ya msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Masime inasema Kulingana na Tarimo, chanzo cha tukio hili ni mazungumzo ya kibiashara aliyoanzisha na watu aliokuwa akiwasiliana nao tangu Oktoba 25, 2024.


 Alikuwa na mipango ya kufanya biashara na watu hao, na alikubaliana kukutana nao katika Hoteli ya Rovenpic, iliyopo Kiluvya, jijini Dar es Salaam. 


Hata hivyo, katika mkutano huo, alikumbana na jaribio la kutekwa, ambalo lilisababisha tukio hilo kutokea. 


Polisi Waanza Uchunguzi



Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa tukio hili na linahakikisha kuwa wahusika watafikishwa mbele ya sheria. 


Msemaji wa Jeshi la Polisi, David  Misime, alithibitisha kuwa uchunguzi unaendelea na hatua stahiki zitachukuliwa kwa wahusika. Akizungumza na vyombo vya habari, Misime alisema:


"Jeshi la Polisi linahakikisha litawakamata watu waliokuwa wakijaribu kumkamata na kumwingiza kwa nguvu kwenye gari mhanga Deogratius Tarimo.


 Uchunguzi unaendelea na hatua zitachukuliwa kulingana na sheria, kwani hakuna aliye juu ya sheria."


Video ya Tukio Inasambaa


Picha mjongeo za tukio hili zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha masahibu ya mhanga, ambapo anasikika akisema kwa sauti kubwa kwamba maisha yake yamo hatarini. Katika video hiyo, mhanga anapiga kelele akisema mara kwa mara:


"Naenda kuuwawa... naenda kuuwawa... siwajui..." (sekunde 0:03 - 0:15).


Watekaji wanamjibu kwa dhihaka:


 "Tutakuua" (sekunde 0:20-0:21), na baadaye wakiendelea kusema: "Sisi ni maaskari" (sekunde 0:36).


Matukio haya yamezua maswali mengi kuhusu hali ya usalama katika maeneo mbalimbali, huku wananchi wakishuhudia tukio hili bila kutoa msaada kwa mhanga.


Maoni ya Watumiaji wa Mitandao ya Kijamii


Wananchi wengi wameonyesha ghadhabu na kutoridhishwa na matukio ya utekaji yanayoongezeka nchini. 


Mtumiaji mmoja maarufu wa mtandao wa X (Twitter), Malisa GJ, aliandika:


"Nisaidieni naenda kuuawa, naenda kuuawa, siwajui hawa, naenda kuuawa," jamaa anapambania uhai wake nje ya Hotel ya Rovvenpec Resort iliyopo Kiluvya madukani, jijini Dar.


 Lakini wananchi wanashuhudia tu, na hawatoi msaada wowote. Yani ilitakiwa hicho kigari kigeuke 'majivu' dakika sifuri lakini watu wanashangaa tu kama vile wanaangalia sinema."


Malisa GJ aliongeza:


 "Angalau huyu aliyechukua video amesaidia kuhabarisha umma, lakini wengine wamesimama tu wakiangalia mwenzao akilalamika kwenda kuuawa. Halafu kesho maiti yake ikiokotwa huko ......watu haohao wangejifanya kusikitika. Watanzania wengi ni wanafiki sana aisee. Ptuu mbaka!"


Aliendelea kusema kuwa wananchi wanapaswa kujitetea wenyewe kwani si rahisi kutegemea msaada kutoka kwa wengine:


"Ukifuatwa na hawa wahuni jitetee kwa nguvu zako zote, its a margin between death and life. Usitegemee watanzania maana wengi ni makondoo tu. Pigania uhai wako mwenyewe. Kama una silaha yoyote itumie kujihami. Usitembee kiboya."


Wasiwasi wa Wanaharakati wa Haki za Binadamu


Mwanaharakati na wakili wa haki za binadamu, Joseph Oleshengay, alikemea vikali vitendo vya utekaji vinavyoendelea nchini. Aliandika kwenye mtandao wa kijamii akisema:


 "Nimejisikia vibaya sana kuona vitendo vya utekaji vinafanyika katika nchi huru na viongozi wala hawajali. Fikiria 'watekaji' wanaongea kwa kujiamini kwamba 'ukigoma kuingia hapo tutakuua' na bado wananchi wanashangaa tu. Pamoja na jamaa kujitetea na kufanikiwa kuokoa roho yake, bado watekaji wamejibu kwa dharau kwamba 'Tutakurudia' maana yake hajakwepa kifo. Amekiahirisha tu."


Oleshengay aliongeza kuwa hali hiyo ni ya kihuzuni na inadhihirisha udhaifu wa mfumo wa usalama na viongozi ambao hawachukui hatua madhubuti. Alisisitiza kuwa ni lazima hatua za dharura zichukuliwe ili kudhibiti vitendo vya kikatili kama hivi.


Mtumiaji mwingine wa mitandao, Martin Maranja Masese, alieleza wasiwasi wake kuhusu hali ya usalama, akisisitiza kuwa wananchi wanahitaji kuwa na uangalifu zaidi. Alisema:


> "Ndugu zangu, utekaji bado upo na watekaji bado wapo. Hapo ni Kiluvya Madukani. Hii ni jana, 11.11.2024 saa nane mchana. Tujitahidi sana kumiliki na kutembea na silaha zozote. Usikubali kufa pekee yako. Wakikuteka, hawakuachi, watakuua. Watanzania ni ng'ombe hawana msaada wowote."


Masese aliwakumbusha wananchi kuwa ni muhimu kujilinda na kuwa na utayari wa kupambana ili kuhakikisha usalama wao, hasa kutokana na hali ya kutokuwepo kwa msaada kutoka kwa wengine katika tukio la utekaji.


Tukio la utekaji la Deogratius Tarimo limezua maswali makubwa kuhusu usalama wa wananchi na ufanisi wa vyombo vya dola katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu. Ingawa Jeshi la Polisi limeanza kuchukua hatua, bado wananchi wanasisitiza umuhimu wa kudhibiti vitendo hivi na kuhakikisha usalama unarejea katika jamii. Vilevile, wananchi wanapaswa kuwa macho na kutafuta njia za kujilinda, kwani usalama wao ni jukumu lao binafsi na waajiriwa wa usalama wanapaswa kuwa na umakini zaidi katika kukabiliana na vitendo vya utekaji vinavyosababisha hofu na maafa.


0 Comments:

Post a Comment