Leo Novemba 17, 2024, Chama cha ACT Wazalendo kimezindua Ilani ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiiji na Vitongoji kwa kipindi cha 2024-2029, ikiwa zimesalia siku chache tu kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba mwaka huu 2024.
Katika uzinduzi huo, ACT Wazalendo imejikita katika masuala muhimu yanayohusu uchumi, ajira, na mazingira ya biashara, ambapo imeahidi kuleta mageuzi makubwa katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa na kuboresha hali ya wananchi, hususan wafanyabiashara wadogo.
Miongoni mwa masuala muhimu yaliyobainishwa kwenye Ilani hiyo ni pamoja na:
Uchumi unaozalisha ajira na kuondoa umaskini: ACT Wazalendo inasema itafanya juhudi za kutengeneza fursa za ajira rasmi na kusaidia wananchi kujiajiri kwa kutoa mazingira bora ya biashara.
Kulinda haki za wafanyabiashara wadogo: Ilani hiyo imeahidi kutunga sheria ndogo zitakazowapa wamachinga hadhi ya kisheria, kulinda shughuli zao na kuboresha mazingira ya biashara.
Kupiga marufuku vitendo vya unyanyasaji: ACT Wazalendo inasema itapiga marufuku kwa halmashauri kutumia vyombo vya dola na mgambo kuwahamisha, kuwabughudhi, kuwavunjia, kuwanyanyasa na kupora wafanyabiashara wadogo.
Uunganishaji wa wafanyabiashara wadogo katika mifumo ya hifadhi ya jamii: ACT Wazalendo inaahidi kuwaunganisha wafanyabiashara wadogo katika mfumo wa hifadhi ya jamii (NSSF) ili kupata mikopo, bima ya afya na kinga dhidi ya ajali na majanga.
Miundombinu ya biashara, Serikali za mitaa chini ya ACT Wazalendo itazingatia kujenga miundombinu ya mijini ikitenga maeneo mahsusi kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo, na kuanzisha masoko maalum kwa siku, saa au mwezi kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali.
"ACT Wazalendo, kupitia Ilani yake, inakusudia kufanya mageuzi makubwa katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa ili ziweze kuwa chombo madhubuti cha kutimiza lengo la kujenga Taifa la wote kwa maslahi ya wote."
"Tutaweka mazingira bora ya biashara kwa kila mtanzania na kuwasaidia wananchi kujiajiri ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu, amesema Zitto Kabwe," Kiongozi wa ACT Wazalendo.
0 Comments:
Post a Comment