Mbowe Amtaka Msigwa Kulipa Fidia ya Bilioni 5 kwa Kumkashifu

 



Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Aikaeli Mbowe, amemtaka aliyekuwa Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, kulipa fidia ya shilingi Bilioni 5 kwa madai ya kumkashifu hadharani. 


Mbowe, kupitia mawakili wake, amedai kuwa Msigwa alisambaza taarifa za uongo kwa nia ya kuchafua sifa na taswira yake mbele ya umma.


Katika barua iliyotumwa na timu ya mawakili wakiongozwa na Hekima Mwasipu, mawakili wa Mbowe wanasema, "Mteja wetu, ndiye Mwenyekiti wa Chama cha Siasa kinachoheshimika kilichosajiliwa chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jina la CHADEMA." 


Mbowe, anatajwa kama kiongozi aliye na mafanikio makubwa kisiasa kitaifa na kimataifa, hivyo matamshi ya Msigwa yameathiri sifa yake kibinafsi na kisiasa.


Mawakili wa Mbowe wameeleza kuwa Msigwa alitoa kauli za uongo kupitia vyombo vya habari na "ulitumia Mteja wetu kama chombo chako cha kutangaza mambo yasiyo ya kweli kwa umma." Wanadai kuwa kauli hizo zililenga kuharibu heshima ya Mbowe kisiasa kwa nia mbaya na kwa makusudi. 


Aidha, Mbowe amempa Msigwa siku tano za kuchapisha ombi la radhi kwenye magazeti mawili makubwa nchini. 


Mawakili hao wameeleza wazi kuwa "Lazima uchapishe kwa uwazi katika ukurasa wa mbele wa magazeti mawili... na kwa namna sawa na jinsi ulivyochapisha taarifa za uwongo, kukiri na kuomba radhi."


Mbowe pia anamtaka Msigwa kulipa fidia ya Shilingi Bilioni 5 kwa kusema "tunakutaka umlipe mteja wetu kiasi cha shilingi bilioni tano za Tanzania kama fidia maalum, mahususi na ya adhabu." 


Fidia hii inatajwa kuwa kwa ajili ya madhara ya kumchafua na kumvunjia heshima mbele ya jamii.


Barua hiyo imeonya kuwa, iwapo Msigwa atashindwa kuchukua hatua hizo ndani ya muda uliotolewa, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake bila taarifa zaidi.

Mchungaji Peter Simon Msigwa aliwahi kuwa Mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuanzia mwaka 2010 hadi 2020. 

Wakati wa kipindi chake cha ubunge, Msigwa alikuwa pia mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, nafasi iliyompa ushawishi mkubwa ndani ya CHADEMA.


Hata hivyo, hivi karibuni, Msigwa alihamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kushindwa kutetea nafasi yake ya Uenyekiti wa Kanda ya Nyasa kwenye uchaguzi wa ndani ya CHADEMA. 


Katika uchaguzi huo, alishindwa na Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu, ambaye aliibuka mshindi na kuwa Mwenyekiti mpya wa Kanda hiyo.




0 Comments:

Post a Comment