Mauaji ya Kiongozi wa CHADEMA Yagubikwa na Sintofahamu: Mbowe Atoa Kauli Kali, Rais Samia Aagiza Uchunguzi wa Haraka



Tukio la mauaji ya Mjumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA Taifa na Msaidizi wa Katibu Mkuu, Mohamed Ali Kibao limezua hisia kali na maswali kuhusu usalama wa viongozi wa kisiasa nchini. Ali Kibao aliuawa kikatili kwa kupigwa sana na hata kumwagiwa tindikali usoni, kama ilivyothibitishwa na uchunguzi wa awali wa mwili wake.


Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA, alizungumza leo tarehe 8 Septemba 2024 akiwa katika Hospitali ya Mwananyamala, akilaani vikali mauaji haya. Akieleza tukio hilo, alisema kuwa Kibao alitekwa nyara kutoka kwenye basi na watu waliokuwa wamebeba silaha na kumfunga pingu kabla ya kumtesa hadi kifo. Mbowe alieleza kwamba kuna mashuhuda walioliona tukio hilo, lakini mwili wa Kibao ulipatikana siku iliyofuata ukiwa umetupwa Ununio, Dar es Salaam. 


"Hatujui kama ni Usalama wa Taifa ama Polisi, lakini waliingia kwenye gari, wakamteka, wakamtesa, na mwili wake ukapatikana asubuhi ukiwa umeteswa sana," alisema Mbowe. "Polisi hawawezi kujichunguza wenyewe, tunahitaji vyombo vya uchunguzi vilivyo huru kuhakikisha haki inapatikana."


Mbowe aliendelea kusema kwamba uchunguzi wa mwili wa Kibao umeonesha alifariki kutokana na mateso makubwa, lakini taarifa rasmi kutoka hospitali inatarajiwa kesho. Aliongeza kuwa iwapo taarifa hiyo itakuwa na utofauti, chama chao kitapinga kwa nguvu zote, huku wanasheria wao wakiendelea kufuatilia mwenendo wa uchunguzi.


Kauli ya Mbowe ilikuja wakati ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alitoa salamu za pole kupitia ukurasa wake wa X, akieleza kusikitishwa sana na tukio hilo. 



Rais Samia aliandika, "Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya mauaji ya kiongozi wa CHADEMA Bwana Mohamed Ali Kibao. Natoa pole kwa viongozi wa chama hicho, familia ya Mzee Kibao, ndugu, jamaa na marafiki."


Rais Samia aliongeza kuwa ameagiza vyombo vya uchunguzi kumletea taarifa kamili kuhusu tukio hili haraka. Aliendelea kusisitiza kwamba nchi ya Tanzania ni ya kidemokrasia na kwamba kila raia ana haki ya kuishi kwa uhuru na usalama. Pia alisisitiza kuwa serikali yake haitavumilia vitendo vya ukatili na mauaji kama haya.


Kwa upande wa Jeshi la Polisi, Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime, alitoa tamko rasmi tarehe 7 Septemba 2024, akithibitisha kupokea taarifa ya kutekwa kwa Kibao kutoka kwenye basi la Tashrif. 



Aidha, Polisi walieleza kwamba mwili wa mwanaume ambaye hakuwa ametambuliwa mara moja, ulipatikana Ununio, Dar es Salaam, na baadaye ukathibitishwa kuwa ni wa Ali Kibao.


Jeshi la Polisi liliendelea kueleza kuwa uchunguzi wa mwili wa marehemu ulifanywa kwa ushirikiano wa familia yake na madaktari bingwa. 


Pia, timu ya uchunguzi toka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai imeongezewa nguvu ili kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa mahakamani. Polisi wameomba yeyote mwenye taarifa za uhakika kuziwasilisha ili kufanikisha uchunguzi.


Tukio hili linaleta taswira mbaya kuhusu usalama wa raia na viongozi wa kisiasa nchini, na linahitaji uchunguzi wa haraka na wa kina. Wakati CHADEMA wakihofia hali hii kuwa dalili ya ukiukwaji wa haki za kisiasa, serikali inahakikisha kwamba uchunguzi utaendeshwa kwa weledi ili haki itendeke.


Mwili wa Kibao utaendelea kufanyiwa uchunguzi zaidi, huku taifa likisubiri taarifa rasmi kesho ili kufahamu kwa undani kuhusu chanzo cha kifo chake. 


Wakati huo huo, wananchi wanatazama kwa makini hatua za serikali katika kulinda haki za raia na kuhakikisha tukio hili halirudiwi tena.

0 Comments:

Post a Comment