Ahukumiwa Miaka 30 Jela kwa Kumbaka Binti Yake wa Kambo

 



Michael John Christopher, maarufu kama Omoro, mkazi wa Nyambiti, Ngudu wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, amehukumiwa kwenda jela miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti yake wa kambo mwenye umri wa miaka 14.



Omoro alifikishwa mahakamani tarehe 9 Aprili 2024 na kusomewa mashtaka ya ubakaji na Mkaguzi wa Polisi Juma Kiparo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi John Chai Jagadi. Mshtakiwa alikana mashtaka hayo na kesi iliahirishwa hadi tarehe 24 Aprili 2024 kwa ajili ya kusikilizwa kwa hoja za awali.


Kulingana na hati ya mashtaka, Omoro anadaiwa kufanya ubakaji huo kati ya tarehe 20 Desemba 2023 na 25 Machi 2024 katika mtaa wa Majengo, Nyambiti, wilaya ya Kwimba, mkoa wa Mwanza. Mkaguzi Kiparo alithibitisha kwamba Omoro alikiuka vifungu vya 130 (1)(2)(e) na 131 (1) vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya sheria marejeo ya mwaka 2022.


Omoro, ambaye ni baba wa kambo wa binti huyo ambaye mama yake alifariki mwaka 2020, alianza uhusiano wa kingono na binti huyo mwaka 2022 walipokuwa wilaya ya Lolya, mkoa wa Mara, na kuendelea baada ya kuhamia Mwanza tarehe 20 Desemba 2023.


Mahakama ilisikia kwamba Omoro aliendelea kushiriki mapenzi na binti huyo hadi tarehe 25 Machi 2024, ambapo binti alikataa kushiriki baada ya ushauri kutoka kwa mama mkubwa, hatua iliyopelekea Omoro kumpiga binti huyo kwa madai ya kumnyima "unyumba".


Uamuzi wa mahakama ulizingatia ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri na bila kusita, Omoro alihukumiwa kwenda jela miaka 30. Omoro alipewa nafasi ya kujitetea lakini madai yake ya kulala chumba kimoja na binti huyo baada ya chumba kingine kurudishwa kwa mwenye nyumba kutokana na kutofikishwa kodi, yalitupiliwa mbali na mahakama.

0 Comments:

Post a Comment