TUCTA Yapongeza Serikali kwa Kuongeza Malipo ya Pensheni kwa Wastaafu
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limetoa pongezi kwa Serikali kufuatia ongezeko la kiwango cha malipo ya mkupuo ya pensheni kwa wastaafu.
Malipo hayo yameongezwa kutoka asilimia 33 hadi 40 kwa wafanyakazi ambao walikuwa wakilipwa asilimia 50 kabla ya mifuko ya pensheni kuunganishwa, na asilimia 35 kwa watumishi waliokuwa wakipokea asilimia 25 kabla ya kuunganishwa kwa mifuko hiyo.
Rais wa TUCTA, Ndg. Tumaini Peter Nyamhokya, alitoa pongezi hizo wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko Morogoro, akieleza kuwa nyongeza hizo zitasaidia kupunguza malalamiko ya wafanyakazi kuhusu kikokotoo cha awali cha pensheni.
TUCTA pia imeishauri Serikali kuangalia upya na kuhakikisha kuna usawa katika nyongeza ya mkupuo ya kikokotoo kwa watumishi wote walioathirika na mabadiliko haya ya Sheria ya Watumishi wa Umma.
"Ni muhimu kuweka usawa katika malipo ya mkupuo kwa watumishi wote wa umma, kwani wote ni kundi moja la wafanyakazi. Mfuko wa pensheni wa PPF ulikuwa imara na kuunganishwa kwake na PSSSF kumesaidia kufungua fursa mpya za pensheni," alieleza Rais Nyamhokya.
Aidha, TUCTA imeishauri Serikali kufanya marekebisho ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa sekta binafsi ili kuhakikisha mabadiliko yanagusa pia wanufaika wa mfuko wa NSSF, siyo PSSSF pekee.

0 Comments:
Post a Comment