Takribani Mahujaji 577 Wafariki Dunia Wakitekeleza Ibada ya Hija



Makka - Takribani mahujaji 577 kutoka mataifa mbalimbali walifariki dunia wakiwa wanatekeleza ibada ya Hija ya mwaka huu, wengi wao kutokana na sababu zinazohusiana na joto kali, kulingana na shirika la habari la Ufaransa, Agence France-Presse.


Shirika hilo limewanukuu wanadiplomasia wa Kiarabu kwamba takribani mahujaji 323 kutoka Misri walifariki dunia wakiwa wanatekeleza ibada ya Hija huko Makka. 


Mmoja wa wanadiplomasia wanaoratibu mawasiliano ya nchi zao alisema kuwa "wote walikufa kutokana na joto" isipokuwa mmoja aliyefariki kutokana na majeraha makubwa wakati wa mkanyagano mdogo kati ya umati wa mahujaji. Idadi hii ilitolewa kutoka chumba cha maiti cha hospitali ya Al-Muaisem huko Makka.


Mapema siku ya Jumanne, Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ilisema kuwa Cairo inashirikiana na mamlaka za Saudia katika kuwatafuta mahujaji wa Misri waliotoweka katika msimu wa Hija.


Ubalozi mdogo wa Jordan wa Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Wageni ulitangaza kuwa umetengeneza vibali 41 vya maziko kwa mahujaji wa Jordan kuzikwa Makka kulingana na matakwa ya familia zao, ikionesha kwamba "hawakuwa sehemu ya ujumbe rasmi wa Hajj wa Jordan."


Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia imesema katika taarifa yake, "Idadi ya mahujaji wa Tunisia waliofariki katika msimu wa Hija imefikia watu 35 hadi sasa, wakiwemo mahujaji 5 waliofika kupitia mfumo wa bahati nasibu ambao serikali inaupitisha kuchagua mahujaji kila mwaka, na 30 waliofika kwa ziara au visa ya Umrah.” Wizara hiyo imethibitisha kuwa ujumbe wa kidiplomasia huko Riyadh na Ubalozi mdogo wa Jeddah unashirikiana na mamlaka husika za Saudia na familia za mahujaji kukamilisha taratibu zinazohusiana na maziko yao.


Mamlaka za Saudia ziliripoti kuwa zimetibu zaidi ya mahujaji 2,000 waliokuwa wanasumbuliwa na uchovu kutokana na joto kali, lakini hawajatoa maelezo zaidi ya idadi hiyo tangu Jumapili na hawajatoa taarifa kuhusu vifo.



0 Comments:

Post a Comment