Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, marehemu Tixon Nzunda, alikuwa kiongozi mwadilifu katika kuwatumikia wananchi na kila mara alikuwa na hofu ya kuwatanguliza wananchi.
Dkt. Mpango alitoa kauli hiyo leo alipofika nyumbani kwa marehemu kusaini kitabu cha maombolezo pamoja na kuifariji familia na wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro. Alisema kuwa marehemu Nzunda ameacha mfano wa kuigwa na watumishi wa umma.
Alisema kuwa anamkumbuka vizuri marehemu kwani alipokuwa Waziri wa Fedha alikuwa anakaa naye sana marehemu akiwa ofisi ya Waziri Mkuu kwenye vikao vyao vya utatu na wafanyakazi, ambapo alikuwa mtu makini sana na mpole.
“Kwa upande wa Serikali, tukio hili limetuumiza sana. Kwa niaba ya Serikali na mimi mwenyewe na Rais ambaye yupo safarini, tunasema poleni sana na niwashukuru kwa moyo wenu toka tukio hili litokee mmekuwa pamoja na familia. Huu ndio Utanzania ninaoufahamu,” alisema Makamu wa Rais Dkt. Mpango.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, akitoa ratiba ya mazishi, alisema Julai 21 saa 4:00 asubuhi mwili wa marehemu Dkt. Tixon Nzunda utafikishwa nyumbani kwake na kufanyiwa ibada fupi ambapo wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro watapata fursa ya kuaga.
"Saa 10:00 jioni, msafara huo utaanza safari ya kuelekea nyumbani kwake jijini Dar es Salaam (Goba) kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ndege iliyotolewa na serikali. Mwili utalala nyumbani hapo ukimsubiria mtoto wake aliyepo nchini India anayetarajiwa kufika Ijumaa saa tatu.
Siku hiyo, wananchi wa Dar es Salaam wakiwemo majirani watapata fursa ya kuaga mwili, na kisha mwili utapelekwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere kwa ajili ya kwenda kijijini kwao mkoani Songwe kwa ajili ya maziko yatakayofanyika Jumamosi Julai 22 mwaka huu," alisema Babu.
Aliongeza kuwa, mwili wa dereva wake Alphonce Edson (54) unatarajiwa kuzikwa Julai 24 nyumbani kwake Mabogini Chekereni.

0 Comments:
Post a Comment