Diane Rwigara Atupwa Nje ya Kinyang'anyiro cha Urais Nchini Rwanda

 Diane Rwigara Atupwa Nje ya Kinyang'anyiro cha Urais Nchini Rwanda 



Mwanasiasa wa upinzani nchini Rwanda, Diane Rwigara, amekumbana na kikwazo kingine katika azma yake ya kugombea urais baada ya kutupwa nje ya kinyang'anyiro hicho kwa mara nyingine tena. Taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Oda Gasinzigwa, zimebainisha kuwa Rwigara hajakidhi vigezo vinavyohitajika kisheria.


Gasinzigwa alifafanua kuwa, Rwigara alishindwa kuwasilisha hati muhimu za rekodi ya uhalifu kama ilivyotakiwa na Tume. Badala yake, alitoa nakala ya kesi, hatua ambayo haikukubalika na Tume. Aidha, Rwigara alishindwa kutoa hati ya kubainisha uraia wake wa asili, badala yake akawasilisha hati ya kuzaliwa. Hii ilikuwa kinyume na mahitaji ya Tume ya Uchaguzi.


Kuhusu idadi ya saini za wafuasi wake, Rwigara alishindwa kukidhi vigezo vilivyowekwa. Gasinzigwa alieleza kwamba kati ya saini zilizowasilishwa, baadhi zilikuwa za watu ambao hawakuwa na vitambulisho halali, na wengine hata walitumia vitambulisho ghushi. Hii ilikuwa ni kinyume cha sheria na taratibu za uchaguzi nchini Rwanda.


Mnamo wiki iliyopita, Rwigara alipowasilisha nyaraka zake za kugombea urais, alionesha matumaini kwamba safari hii ataidhinishwa. Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi iliamua kumfutilia mbali pamoja na wagombea wengine sita kati ya tisa waliojitokeza. Wagombea wengine waliothibitishwa kugombea ni pamoja na rais Paul Kagame, mwenyekiti wa chama cha Green Frank Habineza, na Philippe Mpayimana, mgombea binafsi.


Uchaguzi wa urais unaotarajiwa kufanyika tarehe 14 Julai sasa huenda ukawa na ushindani mdogo, huku idadi ya wagombea ikipungua. Hii inaweza kuashiria kujitokeza tena kwa ushindani kati ya rais Kagame na wagombea wengine wawili, Habineza na Mpayimana.

x

0 Comments:

Post a Comment