RC MAKONDA AMUOMBA RAIS MWINYI KUIUNGANISHA ARUSHA NA ZANZIBAR KIUTALII.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amemuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuiunganisha Zanzibar na Arusha kwenye sekta ya utalii ili kuwezesha mabadilishano ya Watalii wa pande hizo mbili.
Aidha Makonda amemuomba Rais Mwinyi kutangaza fursa na vivutio vya Uwekezaji vilivyopo Mkoani Arusha katika adhma ya kutimiza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuongeza vyumba na Vitanda vya kulala wageni mkoani hapo.
Makonda ametoa maombi hayo leo Mei 17, 2024 wakati Rais Mwinyi akifungua semina ya uwekezaji na elimu ya fedha iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wanahisa wake na Watanzania kuelekea Mkutano Mkuu wa 29 wa Wanahisa utakaofanyika Jumamosi Mei 18, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa huyo ameishukuru benki ya CRDB kwa kuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya Mkoa wa Arusha pamoja na kuuchagua mkoa huo kuwa mwenyeji wa semina na mikutano yao mikuu suala linalowanufaisha wafanyabiashara na wananchi mbalimbali wa mkoa huu,.
Katika majibu yake Rais Dkt. Mwinyi amemuahidi Makonda kuwa atatekeleza maombi yake ipasavyo hasa katika suala la uwekezaji wa ujenzi wa hoteli na nyumba za kulala wageni kutokana na idadi kubwa ya Wawekezaji wanaofika Zanzibar kutaka kuwekeza kwenye ujenzi wa nyumba na vyumba vya kulala wageni na watalii wanaofika nchini.
Akiapishwa mwishoni mwa mwezi Machi Mwaka huu na Rais wa Samia alimuagiza Makonda kukuza utalii wa Arusha pamoja na kuongeza idadi ya vyumba na vitanda vya kulala wageni na watalii kutokana na upungufu mkubwa unaotokana na matokeo chanya ya filamu ya 'The Royal Tour Tanzania' iliyokuwa na nia ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini Tanzania ikiwemo vile vilivyopo mkoani hapa kilipo kitovu cha Utalii Kaskazini mwa Tanzania.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay alisema benki hiyo ikiwa benki ya kizalendo inayomilikiwa na Watanzania kwa zaidi ya asilimia 80, inajivunia kuendelea kukuza thamani ya uwekezaji wa wanahisa wake ikiwamo Serikali ambayo inamiliki asilimia 36 ya hisa katika benki hiyo.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni mwanahisa wa Benki hiyo kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Zanzibar (ZSSF). Dkt. Laay amewakaribisha Watanzania wengine kuwekeza ndani ya Benki ya CRDB ili nawao waanze kunufaika na gawio nono ambalo limekuwa likitolewa na Benki hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela alisema malengo ya semina hiyo ni kuwajengea uwezo Wanahisa wao pamoja na Watanzania wengine ili kuwajengea uwajibikaji wa kifedha na kuongeza ushiriki katika fursa za uwekezaji hususan katika soko la hisa la Da es Salaam.
Kwa kutoa elimu hii Wanahisa wetu pia wanapata kufahamu zaidi faida za kuwekeza katika Benki yao ya CRDB, hivyo basi kuongeza uwekezaji na kupata faida nono zaidi, lakini pia kuwahamasisha na Watanzania wengine pia kuwekeza katika hisa hususan za Benki ya CRDB na kuanza kupata gawio,” aliongezea Nsekela.
Aidha, Nsekela alimshukuru Rais Mwinyi kwa ushirikiano wa kimkakati na mazingira mazuri ya biashara ambayo ndio chachu ya utendaji mzuri wa benki hiyo. Kadhalika, alimhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa Benki ya CRDB itaendelea kuwezesha uchumi wa Zanzibar kwa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo hususan katika kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa za Uchumi wa Buluu.
Katika semina hiyo, mada mbalimbali zilijadiliwa, ikiwa ni pamoja na Ujumuishi wa Kifedha, Uwekezaji katika Hisa, Hatifungani ya Kijani ya Benki ya CRDB, Wosia na Mirathi, pamoja na Kinga dhidi ya Majanga
0 Comments:
Post a Comment