Dola Bilioni 2.2 Zimeahidiwa kwa Ajili ya Nishati Safi Afrika

 Dola Bilioni 2.2 Zimeahidiwa kwa Ajili ya Nishati Safi Afrika


Shirika la kimataifa la Nishati IEA limetangaza kuwa dola bilioni 2.2 za kimarekani zimeahidiwa na makampuni na serikali ili kuboresha upatikanaji wa nishati safi na salama barani Afrika. 


Taarifa hiyo imetolewa baada ya kumalizika kwa mkutano wa kilele uliowakutanisha pamoja viongozi wa mataifa 60 mjini Paris, Ufaransa. 


Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alikuwa miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo.


Zaidi ya watu bilioni mbili duniani hupika kwa kutumia majiko yanayotumia kuni na mkaa, matumizi hayo ya nishati yanatoa moshi ambao unatajwa kuwa ni miongoni mwa sababu kuu ya vifo vya mapema duniani. 


Mbinu hizi za kupikia huathiri mazingira, misitu ambayo ndiyo inayofyonza kaboni hukatwa kwa matumizi ya kuni na wataalam wanasema hali hiyo inachangia ongezeko la joto duniani.


Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la Nishati, karibu theluthi moja ya pesa zinazohitajika ili kubadilisha na kuwahimisha watu duniani kutumia nishati safi na salama ya kupikia zinakusanywa kila mwaka.



Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alizungumza katika mkutano huo wa kilele wa nishati na kueleza mipango ya Tanzania katika matumizi ya nishati safi na salama. 


Dhamira kuu ya Tanzania ni kutekeleza mkakati wa Kitaifa wa miaka kumi ya nishati safi ya kupikia uliozinduliwa hivi karibuni ambao unalenga kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi na salama ya kupikia ifikapo mwaka 2034.



Mwishoni mwa mkutano huo, mkuu wa shirika la IEA, Fatih Birol, alisema mkusanyiko huo umetoa ahadi ya uhakika ya kushughulikia suala hilo ambalo limepuuzwa kwa muda mrefu. 


Benki ya Maendeleo ya Afrika na Shirika la kimataifa la nishati IEA zinatarajia kukusanya fedha dola bilioni 2.2 kwa ajili ya kuongeza uwekezaji katika masuala ya nishati safi na salama kwa mwaka huu.



0 Comments:

Post a Comment