TIRA KANDA YA KASKAZINI YAWAKUTANISHA MAWAKALA WA BIMA

 TIRA KANDA YA KASKAZINI YAWAKUTANISHA MAWAKALA WA BIMA  





MAWAKALA  wa bima wa kanda ya kaskazini wametakiwa kufanya shughuli zao kwa kuzingatia weledi na  kufuata sheria na kanuni zilizopo kwani wao ndio wanaotegemewa zaidi katika kufanikisha shughuli mbalimbali za bima.





Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Kaimu  Meneja wa  Mamlaka ya usimamizi wa Bima  kanda ya kaskazini, Gladness Lema wakati akizungumza  na mawakala hao katika kikao kilichofanyika katika ofisi zao zilizopo mkoani Arusha .




Amesema kuwa ,lengo kuu la kutoa mafunzo hayo ni kujadili kuhusu kutekeleza miongozo mbalimbali ya bima ambayo mamlaka imeshaileta sokoni na namna ambavyo wanaweza kuongeza wigo wa biashara  sambamba na kukumbushana wajibu wao na kuweza kusilikiza  changamoto mbalimbali na kuweza kupatiwa ufumbuzi wa moja kwa moja.


Gladness amesema kuwa ,mawakala hao wanatakiwa  kusimamia vizuri  taaluma zao hususani wanapotoa  leseni na kuhakikisha wanafuata weledi na kamwe wasikubali  kudanganyika  kabisa .


"Heshima ya soko letu ni sisi wenyewe hivyo hatuna budi kuhakikisha kuwa tunazingatia  weledi katika  kufanikisha shughuli zetu na kamwe tusikubali kudanganyika  wakati wa kutoa haki kwa wateja wetu tuwaeleze  ukweli ."amesema .


Amesema kuwa baada ya mkutano huo wanatamani kuona soko la bima linakuwa na ustawi ,solo Kenya faida linalovutia wawekezaji na linalokuwa hasina rushwa na kukuza pato la nchi yetu.


Ameongeza kuwa,mkutano huo ni muhimu sana katika kujengeana uelewa wa pamoja kwa kuzingatia mawakala ndio wasajiliwa wengi kuliko wengine  hivyo kufanya kuwa mawakala ni jeshi kubwa .


"Kwa Tanzania nzima  kwa mwaka 2022 tulikuwa na  mawakala 922 kwa kanda ya kaskazini tunao mawakala 136 kwa mwaka 2023 ikiongozwa na mkoa wa Arusha wenye mawakala 88 ikifuatiwa na Kilimanjaro ambapo kuna mawakala 27 na Tanga mawakala 21.



Aidha amefafanua kuwa ,kupitia mkutano huo watapata manufaa makubwa sana na utatoa mwanga wa maeneo ya kuboresha na kuongeza nguvu ili  iwe biashara ya kutamaniwa kufanywa na kila mtu kwa kuonyesha namna ya kuongeza mapato katika wigo  mpana  kibima na kuboresha utendaji kazi wa kila siku.


Naye Mhasibu kutoka Hazina ndogo Arusha , Izhaki Daniel akifungua mkutano huo amewataka mawakala hao kuifanyia  kazi elimu hiyo na kuhakikisha wanafanya kazi kwa uadilifu  mkubwa huku wakifuata  taratibu na sheria za mamlaka hiyo ili kuzuia ukiukwaji .


"Naishauri mamlaka iendelee kutoa elimu kwa bidii kwa mawakala zaidi ili waweze kupata uelewa  wa kutosha na wasisite kuwachukulia hatua za kisheria  na kutoa adhabu kali kwa mawakala wote wanaokikuka sheria "amesema.



Kwa upande wake Afisa leseni mwandamizi kutoka Brela ,Rehema Kionaumela amesema kuwa wameweza  kutoa elimu mbalimbali kupitia kikao hicho na kuweza kuwaelimisha  mawakala hao kazi zinazofanywa  na Brela ,huku wakisisitiza  mawakala ambao hawajajiandikisha na Brela wahakikishe wamesajili  kampuni  na biashara zao ili waweze kupata cheti cha kampuni na majina ya biashara.


"Napenda kutumia fursa hii kuwataka wale mawakala wote wanaofanya biashara zenye sura ya kitaifa na kimataifa kuhakikisha wanakata leseni Brela ili waweze kufanya shughuli zao kwa umakini huku wakifuata sheria na kanuni zilizopo. "amesema  


Nao Baadhi ya mawakala wakizungumza katika mkutano huo waliomba uongozi wa Tira kutoa mafunzo mara kwa mara ili kuwajengea uwezo zaidi sambamba na kuweza kukumbushana wajibu wao na kuweza kuondokana na changamoto  mbalimbali .



0 Comments:

Post a Comment