Jeshi la Polisi Dar es Salaam Wawakamata Watuhumiwa wa Kuingiza Vifaa vya Mtandao Bila Kibali

 Jeshi la Polisi Dar es Salaam Wawakamata Watuhumiwa wa Kuingiza Vifaa vya Mtandao Bila Kibali



Kikosi kazi maalum cha Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kimetangaza kukamata watu wawili kwa tuhuma za kuingiza vifaa vya mawasiliano ya intaneti nchini bila kufuata taratibu za kisheria. Watuhumiwa hao ni Claudian Makaranga (28) mkazi wa Kawe na Hongliang Yang (35) raia wa China, mkazi wa Kigamboni.


Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum SACP Jumanne Muliro ameeleza kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakijitangaza kuuza vifaa na kutoa huduma ya mtandao kupitia akaunti ya Instagram yenye jina la @Starlink. Baadhi ya vifaa hivyo vilishauzwa na kutumika katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, hatua ambayo ni kinyume cha sheria kwani vifaa hivyo havikuwa vimeidhinishwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).


Kamanda Muliro amewataka wananchi kuwa makini na kununua vifaa vya mawasiliano kutoka vyanzo halali na vilivyoidhinishwa na mamlaka husika ili kuepuka kuvunja sheria na kukumbwa na hatua za kisheria.


Tukio hili linawakumbusha wananchi umuhimu wa kufuata taratibu na sheria za nchi wanapofanya shughuli za mtandaoni ili kuhakikisha usalama na utulivu wa nchi unadumishwa. Tutakuwa tukifuatilia kwa karibu maendeleo ya kesi hii na kutoa taarifa zaidi kadri zinavyopatikana.

Chanzo EATV


0 Comments:

Post a Comment