Mkutano wa SADC kujadili Mlipuko wa Kipindupindu:


Mkutano wa SADC kujadili Mlipuko wa Kipindupindu: Waziri Mkuu Majaliwa Awasilisha Mapendekezo ya Tanzania





Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa dharura wa SADC uliofanyika mtandaoni, ukihusisha nchi wanachama wa Jumuiya hiyo. Ajenda kuu ilikuwa kujadili mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika eneo la SADC.


Mkutano uliofunguliwa na Rais wa Angola, Joao Manuel Lourenco, ulishuhudia Waziri Mkuu Majaliwa akipendekeza hatua jumuishi za kukabiliana na kipindupindu, kuhusisha sekta zote mtambuka. Tanzania inasisitiza umuhimu wa ushirikiano wa sekta za maji na mipango miji kwa suluhisho la kudumu.


"Tunashauri nguvu kubwa ielekezwe katika kuboresha mifumo na upatikanaji wa maji safi na salama," alisema Majaliwa, akiongeza wito kwa jamii kuchukua tahadhari na kuzingatia kanuni za usafi (WASH).


Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu; Waziri wa Maji, Jumaa Aweso; pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk.


Rais Lourenco alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mawasiliano baina ya nchi wanachama, hasa katika maeneo ya mipakani, na kuwekeza katika teknolojia na tafiti kwa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.


Marais walioshiriki ni Phillipe Nyusi (Msumbiji), Lazarus Chikwera (Malawi), Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe), Haikande Hichelema (Zambia), Felix Tshisekedi (DRC), pamoja na wawakilishi wa nchi nyingine za SADC.

0 Comments:

Post a Comment