Matukio mbalimbali Maandamano Chadema Mwanza

 Matukio mbalimbali Maandamano Chadema Mwanza 



Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ameongza maandamano ya amani jijini Mwanza yaliyoanzia Igoma, Ilemela na Buhongwa mpaka  viwanja vya Furahisha jijini humo.







Maandamano hayo yenye misafara mitatu kwa upande wa Igoma yameongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho  Mbowe, msafara wa kutokea Buhongwa kupitia barabara Kuu ya Kenyatta umeongozwa na Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu, huku Katibu Mkuu John Mnyika msafara wake ukitokea barabara ya Airport Ilemela.


Kilele cha Maandamano ya amani kimefanyika  katika viwanja wa Furahisha ambapo viongozi wa Chadema wanazungumza na wananchi na wafuasi wa chama hicho.



Akizungumza Mbowe amesema maandamano yanalenga kuishinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau mbalimbali kuhusu masuala ya uchaguzi.

Vilevile chama hicho kinaitaka serikali iondoe bungeni miswaada inayohusu vyama vya siasa na uchaguzi, ambayo ni muswada wa Marekebisho ya Sheria za Vyama vya siasa na Sheria ya gharama za Uchaguzi.

Badala yake Serikali iwasilishe muswada wa kukwamua mchakato wa Katiba mpya kwa kuzingatia mwafaka wa kitaifa. Kwani Chadema inaamini, “serikali imepuuza maoni yaliyotolewa na Kikosi Kazi pamoja na wadau mbalimbali.”

Kadhalika, Chadema imeitaka Serikali iwasilishe bungeni muswada wa kufanya marekebisho ya mpito ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ili uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 na ule mkuu wa 2025 uwe huru na haki.

Suala la gharama za maisha pia limekuwa ajenda ya maandamano: “Tunataka serikali ipeleke mpango wa kuwakwamua wananchi na hali ngumu ya maisha bungeni, ikiwa ni pamoja na kushusha bei ya bidhaa muhimu au kuweka ruzuku katika baadhi ya bidhaa,” amesema Mbowe.

0 Comments:

Post a Comment