Maandamano ya CHADEMA Yavutia Maelfu Arusha

 Maandamano ya CHADEMA Yavutia Maelfu Arusha



Maelfu ya watu leo wamejitokeza katika maandamano yaliyoandaliwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Arusha.


Maandamano hayo yalianza asubuhi katika vituo vya TANAPA, Morombo, na Kwa Mrefu na kufikia kilele chake katika viwanja vya reli vya Unga Limited jijini Arusha.


Waandamanaji hao, waliotembea umbali wa zaidi ya kilomita 30, hawakurudi nyuma hata baada ya kunyesha kwa mvua kubwa. Wakiimba nyimbo za hamasa, walitoa kilio chao kuhusu hali ya siasa na uongozi nchini.


Akiongoza maandamano hayo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisisitiza azma ya chama hicho kudai mabadiliko na haki kwa wananchi. Alilaani matumizi mabaya ya kodi za umma na kuitaka serikali ichukue hatua za haraka.



Viongozi wengine wa CHADEMA akiwemo Makamu Mwenyekiti Bara,  Antipas Lisu na Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, wakisisitiza umuhimu wa serikali kusikiliza kilio cha wananchi na kuchukua hatua za haraka.


Maandamano haya yalivutia watu kutoka maeneo mbalimbali ya Arusha na hata mikoa jirani. 

Wananchi wameahidi kuendelea kupaza sauti zao hadi haki itakapopatikana na maisha bora kwa kila Mtanzania yatakapohakikishwa.


 "Licha ya kutembea kilomita zaidi ya 30 huku mvua zikinyesha takriban masaa mawili bado watu hawakukubali kusitisha maandamano taswira hii inaashiria Watanzania wanataka mabadiliko na sio kudanganywa kwa siasa za uongo," Amesema Mbowe. 

Amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuacha kufuja kodi za wananchi kusafiri kwenda nje makundi ya watu suala ambalo ni ubadhilifu wa mali za umma na kuwaumiza walipa kodi wanaoishi maisha duni.

 "Mimi nashangaa Samia akisafiri unamuona Kikwete (Rais Mstaafu, Jakaya Mrisho) pembeni yake kwani Kikwete amekuwa nani ? Kikwete ametumika miaka yake kumi madarakani anatakiwa akapumzike aache kufuja kodi za wanyonge kwa sababu yeye ana mshahara na ana marupurupu," amesema Mbowe. 


Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Lissu amesema Watanzania wamechoka kwa kutosikilizwa na serikali iliyopo madarakani hivyo maandamano yataendelea mpaka haki ipatikane.

 "Jeshi la polisi nchini linatakiwa kuwalinda wananchi na sio kuwasonga na kuwagasi kama ambavyo wamefanya Leo wakati maandamano yaliyoanza katika kituo Cha Morombo mapema Leo asubuhi," ameeleza Lisu.


Amesema kuwa mfumuko wa bei kwa bidhaa muhimu kama sukari ni hatari kubwa kwa wananchi wengi wenye Hali ya chini na wenye kipato Cha chini. Hata hivyo Lisu amesema kwamba viongozi wa serikali wanajilimbikizia mali kwa kujinunulia magari ya kifahari kwa kutumia kodi za wananchi badala ya kununua magari ya ya kubeba wagonjwa na kununua vitendanishi vingine. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Lema ameitaka serikali ya Mkoa wa Arusha kuachana na vikwazo na sababu zisizo za msingi pindi maandamano yanapoitishwa, kwani maandamano ni ishara inayoashiria wananchi kuionyesha serikali kuwa wamechoka na wanataka haki. 


"Sauti ya wengi ni Sauti ya Mungu naamini serikali itafanyia kazi kwa hiki kilichofanyika leo" amesema Lema.

Kwa upande wake, wakili,  Boniface Mwabukusi amesema maandamano hayo ni hatua kamili ya kupata kinachotakiwa na Watanzania wote. 

"Nawapongeza sana kujitokeza na kuvumilia licha ya mvua kubwa zilizonyesha lakini bado mliendelea kwa sababu mnachokitaka ni maisha Bora na upatikanaji wa huduma za Jamii ambazo bado hazipatikani kutokana na Chama Cha Mapinduzi kilichoko madarakani lwa zaidi ya miongo sita sasa, ".amesema Mwabukusi na kuongeza.

"Naendelea kuwatumia Salam na kuwasisitiza wenzetu wa CCM wasirudie kufanya walichokifanya katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 bali tunataka uhuru na haki itendeke katika uchaguzi ujao wa 2025 vinginevyo tutatafuta haki yetu kwa namna yoyote"  

Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya kisiasa wameelezea uwepo wa  wa Pengo la Kijinsia katika Maandamano ya CHADEMA Arusha: Kutokushirikishwa kwa Wanawake.

Maandamano yaliyoandaliwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Arusha yalivutia maelfu ya watu kutoka maeneo mbalimbali, wakitoa kilio chao kuhusu hali ya siasa na uongozi nchini. 

Hata hivyo, uchambuzi wa kina wa maandamano hayo unaonyesha pengo kubwa lililojitokeza kwa wanawake  kutokushirikishwa katika kutoa maoni yao, licha ya kushiriki kwao kikamilifu katika maandamano.

Akiongelea hali hiyo mwanahakarakati wa haki za binadamu, Mary Mushi anasema ni wazi kuwa wanawake walikuwa sehemu muhimu ya maandamano hayo, wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita 30 pamoja na wanaume, huku mvua kubwa ikinyesha. 

Ushiriki wao unaonyesha nia yao ya dhati ya kutafuta mabadiliko na haki kwa wananchi wote wa Tanzania. Hata hivyo, wakati wa kutoa maoni na kutoa matamko rasmi, sauti za wanawake zilionekana kutokuwepo kabisa.


Mary alisema kuwa wakati wa maandamano, viongozi wakuu wa CHADEMA walijitokeza kutoa hotuba na maoni yao kuhusu hali ya kisiasa na kiuchumi nchini. 

" Hakuna mwanamke aliyepata nafasi ya kutoa maoni licha ya Chama hicho kuwa na viongozi wanawake mpaka kwenye Kamati Kuu ya Chama hicho, hali inayojenga picha ya kutokuwepo kwa uwakilishi sawa wa kijinsia katika ngazi za juu za maamuzi," alisema Mary



Kwa upande wake Bakari Mollel ambaye alishiriki maandamano hayo alisema kuwa wanawake ni sehemu muhimu ya jamii na wanakumbwa na changamoto nyingi zinazohitaji sauti yao kusikika ili kupata suluhisho bora.

Maandamano ya CHADEMA yalikuwa na lengo la kudai haki na mabadiliko kwa Watanzania wote, lakini pengo lililojitokeza katika kutokushirikishwa kwa wanawake katika kutoa maoni yao linaonyesha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanywa ili kufikia usawa wa kijinsia.



0 Comments:

Post a Comment