TANESCO YAPEWE SIKU 30 KUFANYA MAREKEBISHO YA MASHINEUMBA ZENYE KASORO

 TANESCO YAPEWE SIKU 30 KUFANYA MAREKEBISHO YA MASHINEUMBA ZENYE KASORO


Serikali imetoa siku 30 kwa Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) ili kuhakikisha wanafanyia kazi dosari na mapungufu yote yaliyopo kwenye mashineumba zenye kasoro ili  kuendelea kutoa huduma ya umeme wa uhakika nchini.



Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa upanuzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Mbagala pamoja na njia ya msongo wa Kilovoti 132 kutoka Kituo cha kupoza umeme cha Ilala kwenda Kurasini kwa kutumia waya zinazopita ardhini.



“TANESCO nawapa siku 30 muhakikishe mnafanya marekebisho ya miundombinu ya umeme zikiwemo mashineumba zenye kasoro kwa kuzifungia vifaa vinavyostahili ili wananchi waendelee kupata umeme wa uhakika bila changamoto yoyote," amesema Kapinga.


Amesema kuwa ni muda sasa kwa watendaji wa TANESCO kubadilika na kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia taaluma zao ili waendelee kulinda miundombinu ya umeme ambayo serikali inawekeza fedha nyingi kwa lengo la kufikisha huduma bora ya umeme kwa wananchi.


Naibu Waziri Kapinga amesema wataalam wa TANESCO wahakikishe wanafikisha vifaa vyenye ubora kila mahali ili mafundi wanapofika katika maeneo mbalimbali kufanya marekebisho wavikute.


Pia, amesisitiza kuwa mradi wa ujenzi wa waya wa ardhini kutoka Ilala hadi Kurasini wa Kilovolti 132 wenye urefu wa kilomita saba unaendelea vizuri.


Aidha, utekelezaji wa mradi huu ulianza January 31, 2023 na unatarajia kukamilika mwezi Machi 2024 na unatekelezwa na kampuni ya TBEA kutoka China kwa gharama ya Dola za Marekani 5,996,666 na Mradi huu unafadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100.

0 Comments:

Post a Comment