Mtuhumiwa wa Mauaji ya Beatrice Akamatwa Baada ya Kujaribu Kujiua Arusha

Beatrice Minja enzi za uhai wake, kushoto akipatiwa matibabu kwenye hospitali ya KCMC baada ya kujeruhiwa.

Jeshi la Polisi nchini limetangaza kukamatwa kwa Lucas Paul Tarimo, mshukiwa mkuu wa mauaji ya Beatrice James Minja, aliyefariki dunia Desemba 27, 2023, baada ya kujeruhiwa kwa kuchomwa visu mnamo Novemba 12, 2023.


Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Msiime, ameeleza kwamba Tarimo amekamatwa leo Desemba 31,2023 alfajiri katika kijiji cha Jema, kata ya Oldonyosambu, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha. Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alikuwa akijiandaa kukimbilia nchi jirani, ambayo haikutajwa, na ametoa shukrani kwa ushirikiano wa wananchi wa kata hiyo.


Msiime alisema, "Tunawashukuru sana wananchi wa kata hiyo kwa ushirikiano mkubwa waliotoa kwa jeshi la polisi hadi kufanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo." Hata hivyo, baada ya kugundua kuwa anakaribia kukamatwa, Tarimo alijaribu kujiua kwa kunywa sumu ya kuua wadudu.


Akizungumzia hali ya mtuhumiwa, Msiime alisema, "Mtuhumiwa amepatiwa huduma ya kwanza na yupo vizuri. Taratibu za kisheria zinaendelea kufuatiliwa kuhusiana na kesi hii."

Awali https://habaritanzaniagracemacha.blogspot.com/2023/12/jeshi-la-polisi-latoa-ufafanuzi-mauaji.html

Kifo cha Beatrice Minja kimeleta mshtuko kwa jamii, na sasa macho ya umma yanatazamia kwa karibu maendeleo ya kisheria yatakayojitokeza katika kesi hii ya mauaji hasa ikizingatiwa kuwa mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwa mfanyakazi wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda na mbunge wa Rombo.



Hata hivyo jana Desemba 30,2023 kiongozi huyo tayari ameshajitokeza kwenye kituo cha ITV  na kukana kumfahamu ‘shamba boy’ huyo.

Tarimo anadaiwa kumchoma visu na kumsababishia umauti Beatrice mkazi wa Rombo mkoani Kilimanjaro ambaye alikuwa na mahusiano naye ya kimapenzi kabla ya wawili hao kuachana.



0 Comments:

Post a Comment