WAZAZI NA WALEZI WAKUMBUSHWA KUPELEKA WATOTO SHULE

 


Na Mwandishi Wetu- Kilimanjaro

Wazazi na walezi nchini wametakiwa kuhakikisha watoto wao waliofikia umri wa kwenda shule wanapelekwa ili kupata elimu itakayowawezesha kuwa wataalam wa fani mbalimbali pamoja na kutimiza ndoto zao.



Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi wakati akizungumza katika  mkutano wa hadhara Kata ya Mroe, Jimbo la Same Mashariki ikiwa ni ziara yake katika Jimbo hilo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho.



Mwenyekiti huyo amesema baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakizuia watoto wao kwenda shule huku wanaume wakitumikishwa katika shughuli za kilimo au kuchunga ng’ombe na wale wa kike wakilazimishwa kuolewa.



“Wazazi na walezi pelekeni watoto shule Serikali inahitaji wataalam wengi zaidi katika fani mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji, barabara na nyinginezo. Pia mkumbuke juhudi hizi zinafanywa na Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kila mtoto apate elimu bora na ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chma chetu,”Amesema Mwenyekiti huyo.



Vilevile amewasisitiza wanafunzi kuepuka vishawishi kwa kuwa na msimamo, kutojihusisha na makundi mabaya hatua itakayowafanya kushindwa kutimiza ndoto zao na hatimaye kujiingiza katika matendo ya uhalifu na kuzalisha jamii tegemezi.

“Msikubali kukatishwa tamaa na marafiki wabaya, watoto wakike wapewe fursa ya kusoma watimize ndoto zao hapo tutapata wakurugenzi, madaktari, Mawaziri msiwafanyie hayo mnayoyafanya ni machukizo mbele ya Chama, Serikali na hata Mwenyezi Mungu,”Ameeleza.




Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo ametoa kadi za Chama kwa baadhi ya wanachama waliorudi CCM wakitoka katika vyama vingine wakisema lengo la kufanya uamuzi huo ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita.




Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum, Ummy Nderiananga amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ambayo iko ndani ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kukuza uchumi wa Taifa.



“Sisi Serikali kupitia Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tunaendelea kutekeleza ilani na niwahakikishie kazi inaendelea vizuri hakuna kitakachosimama, tunafanya kazi usiku na mchana kwa sababu nyinyi wananchi ndiyo mmetupa kazi. Pia niwatoe hofu mnapoona wageni wanakuja kuwekeza nchini ni kutokana na mahusiano mazuri aliyonayo Rais wetu na Nchi zingine na wadau wa maendeleo,”Amefafanua . Ummy.


Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Anna Kilango (kushoto) akifafanua jambo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Mroe na (kulia) ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi wakati wa ziara ya Mwenyekiti huyo aliyoifanya katika Jimbo hilo kukagua utekelezaji wa ilani ya Chama.


Naye Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki Mhe. Anna Kilango amebainisha kwamba Serikali inaendelea kuboresha miradi mikubwa ya maji akisema kuwa licha ya changamoto kubwa ya maji katika Jimbo la Same Mashariki bado Serikali ina nia njema ya kumtua ndoo mama kichwani ili wananchi wake waendelee kufanya shughuli za uzalishaji na kukuza uchumi.

“Nikiri Jimbo langu linakabiliwa na uhaba wa huduma muhimu ya maji lakini bado Serikali haijatuacha inatoa fedha za kuboresha miundo mbinu ya maji hatua itakayosaidia wananchi wangu wa Same Mashariki kufanya kazi zao kwa amani. Pia tunamshukuru sana mama kwa kuendelea kupigania na kuhubiri amani katika Nchi yetu,”Amepongeza Mbunge huyo.


Aidha Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Kilimanjaro, Adam Simba amehimiza kufanywa kwa ufuatiliaji wa karibu wa miradi inayofanya na Serikali ili  kubaini hatua iliyofikiwa, changamoto  na namna ya kuzitatua kwa maendeleo ya Taifa.


0 Comments:

Post a Comment