Kamisaa wa Sensa Ahimiza Waandishi Kutumia Takwimu za Sensa ya 2022


KAMISAA wa Sensa ya Watu na Makazi Nchini, Anne Makinda, amewahimiza waandishi wa habari kutumia kwa umakini takwimu zilizokusanywa katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ili kuchangia katika maendeleo ya jamii na kusaidia wadau mbalimbali kuwekeza katika maeneo yenye mahitaji.



Ameyasema hayo wakati wa semina ya uwasilisha, usambazaji, na uhamasishaji wa matumizi ya matokeo ya sensa,iliyofanyika jijini Arusha, Oktoba 24,2023  iliyoshirikisha waandishi wa habari 110 kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, na Manyara,  

Makinda ambaye pia ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisisitiza umuhimu wa takwimu za sensa kama chombo cha kueleza ukweli na kuonyesha maeneo yanayohitaji huduma na uwekezaji.

Makinda aliongeza kwa kusema, "Waandishi wa habari msiwe na hofu, maana mkihofia, nchi haitasonga mbele. Kila mmoja wetu atimize wajibu wake, viongozi na wanahabari, kwa kuzingatia takwimu sahihi na siyo zile za uongo."

Kamisaa huyo wa Sensa alisisitiza kuwa taarifa za sensa zinaeleza ukweli wa mambo na kuonyesha maeneo yenye uhitaji wa huduma. Kwa kutumia takwimu hizo, wadau na serikali wanaweza kuona maeneo ya kuwekeza na kushughulikia changamoto zilizopo.

Makinda alitoa wito kwa waandishi wa habari kuhakikisha wanahamisha taarifa hizo kwa wananchi kuanzia ngazi ya kaya ili ziweze kusaidia katika kufanya maamuzi ya uwekezaji katika shughuli za maendeleo.


Akifungua semina hiyo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, aliwaambia waandishi wa habari kuwa jukumu lao ni muhimu katika kusambaza taarifa sahihi za takwimu zinazotokana na sensa. Aliwashauri pia kuwafikia vijana wa vyuo vikuu, ambao wana hamu ya kujifunza mambo mapya.

Semina hiyo ililenga kuwajengea uelewa wa kuandika na kuripoti kwa usahihi habari zinazohusiana na takwimu zilizokusanywa katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 na kutoa mwanga wa jinsi taarifa hizi zinaweza kuchangia maendeleo ya taifa

0 Comments:

Post a Comment