Serikali Yawekeza Bilioni 80 kusambaza Umeme Vijijini Mkoani Kagera"





Serikali imezidi kuimarisha upatikanaji wa umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), huku ikiwekeza jumla ya shilingi bilioni 80 kwenye miradi ya usambazaji wa umeme mkoani Kagera. Hatua hii muhimu inalenga kuwaletea wananchi nishati bora na kuchochea maendeleo katika maeneo ya vijijini.



Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, amesema hayo  leo, Septemba 27, 2023, wakati Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Dkt. Doto Biteko, walipowasha umeme katika vijiji vya Mubaba na Nyantakara, Wilaya ya Biharamulo, mkoani Kagera.


Akifafanua, Mhandisi Saidy alitaja miradi inayotekelezwa kuwa ni pamoja na REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, upanuzi wa umeme pembezoni mwa miji, ujazilizi, kupeleka umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo, na kutoa umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.


Kati ya vijiji vyote 662 vilivyopo mkoani Kagera, asilimia 77.3 ya vijiji, sawa na vijiji 512, vimeshapatiwa huduma ya umeme kupitia miradi ya awali kama vile REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, REA Awamu ya Pili na REA Awamu ya Kwanza.


Wakala wa Nishati Vijijini umejitahidi kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali kwenye mkoa wa Kagera, ukilenga kuwapelekea wananchi nishati, na hivyo kuboresha huduma za jamii katika maeneo ya vijijini na vijiji-miji. Hatua hii inaonesha dhamira ya serikali katika kufikia malengo ya kutoa nishati bora kwa kila mwananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Endelea kufuatilia ili kujua matokeo ya jitihada hizi muhimu

0 Comments:

Post a Comment