RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kuwa anataka kuona mashirika ya umma yasiyotegemea kuchukua kodi za wananchi serikalini ili kujiendesha ambapo ameyataka yajiendeshe kwa faida ili kuchangia bajeti ya nchi .
Aidha amesema kuwa
lengo hilo litafikiwa baada ya kufanyika mabadiliko ya kiutendaji, kisera na
kisheria ikiwemo kuondoa kuingiliwa kisiasa katika utendaji wa mashirika haya,
sheria za manunuzi, na mikataba sahihi ya kiutendaji kati ya serikali na wale
tunaowakabidhi kuendesha mashirika haya.
Rais Samia ameeleza
hayo leo tarehe 19 Agosti, 2023 wakati akifungua kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na
Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma jijini Arusha.
‘Mageuzi na maboresho
haya kwa mashirika yetu ya umma ni ya lazima, na ninawapa baraka zangu zote na
ushirikiano katika utekelezaji wake. Watendaji tuliowapa dhamana ya kuongoza
mashirika haya waende na kasi hii ya mageuzi ili kufikia malengo ya Serikali
katika kuwatumikia Watanzania. Wale wasioweza, mlango wangu uko wazi, waje
waniambie, ‘Mama siwezi’,” amesema Rais Samia na kuongeza
…Mjizatiti kuzalisha
na kufanya mashirika yasimame, kama ni shirika la huduma litoe huduma
tunayoiona , kama ni shirika la biashara litoe biashara tunayoiona..Lakini
mashirika yamekuwa ni sehemu ya kula raha, na ndio maana juzi tulikuwa
tunazungumza Waziri wa Utumishi akasema jamani pale kwangu Utumishi nina vita,
kila mtu anataka kuhama Serikalini kwenda kwenye mashirika, kisa kuna
marupurupu mazuri, mishahara minene lakini hakuna tija kwa Serikali, sasa
hatuwezi kwenda hivyo,".
Rais Samia amesema
kuwa ndoto ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu, Julius Nyerere katika kuanzishwa
kwa mengi ya mashirika hayo ilikuwa kuona yanamilikiwa na umma wa Watanzania,
yanaendeshwa kwa tija na yasiyo mzigo kwa wananchi.
“Hivi sasa tuna
mashirika, taasisi na wakala za umma takribani 248, zenye mtaji wa shilingi
Trilioni 73 lakini zinachangia chini ya asilimia 4 ya bajeti ya nchi yetu. Japo
yapo baadhi ya mashirika yanayojitahidi kufanya vizuri, bado hatujafikia ndoto
njema ya Baba wa Taifa kwa nchi yetu, na tunahitaji kufanya maboresho na
mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa mashirika haya ili kutoka hapa tulipo,”
amesisitiza Rais Samia.
0 Comments:
Post a Comment