Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji: Kuangazia Changamoto za Mkoa wa Arusha



Kila tarehe 6 ya Februari, dunia inaungana kwa lengo moja kubwa - kupinga ukeketaji na kuelimisha jamii kuhusu madhara yake. 

Ukeketaji ni mila inayoendelea kufanyika katika sehemu nyingi za dunia na inajumuisha kuchana au kuondoa sehemu za nje za viungo vya uzazi wa wanawake. Matokeo yake ni madhara makubwa ya kimwili na kisaikolojia. 

Mkoa wa Arusha, na hasa wilaya za Longido, Monduli, na Ngorongoro, unakabiliwa na changamoto za pekee linapokuja suala la ukeketaji. Mila hii inaendelea kuwa tishio kwa afya na haki za wasichana na wanawake katika eneo hili.

Mbinu Mpya za Ukeketaji Mara nyingine, jamii za wafugaji wa Kimasai katika wilaya hizi za Arusha wamekuwa wakibadilisha mbinu za ukeketaji ili kukwepa sheria na ukaguzi wa vyombo vya dola. 

Moja ya mbinu hizi ni kukeketa watoto wachanga, mara nyingine hata kabla ya kuzaliwa. 

Hii ni kutokana na imani kwamba watoto hawawezi kutoa ushahidi wa kukeketwa na hivyo kuwa na kinga dhidi ya sheria.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya  kuibuka matukio ya ukeketaji watoto, Wilaya ya Longido mkoa wa Arusha, baadhi ya wazazi na maafisa wa serikali wilaya ya Longido walisema bila hatua kali kuendelea kuchukuliwa ukatili huu dhidi ya watoto hautakoma.

Baadhi ya wakazi wa Wilaya hiyo ambayo asilimia 95 ya wakazi ni wafugaji wa Jamii kimasai wameeleza kuwa kutokana na jitihada na serikali wilaya Longido kudhibiti watoto wakiwa shuleni kufanyiwa ukeketaji baadhi ya wazazi sasa wanakeketa watoto.

Paulo Orkediaye mkazi wa Kijiji Cha Oltepesi anasema licha ya elimu kuendelea kutolewa baadhi ya wazazi wanakeketa watoto wachanga kwa siri.


"Hi tabia ni mbaya Sana tunatoa elimu kupinga ukeketaji lakini baadhi ya wazazi wanaendelea kukeketa mbaya zaidi wanakeketa watoto wadogo ambao awajitambui na awana ueewa" alisema

Sarah Ole Varoya  (si jina halisiPmkazi wa Olbomba alisema mkakati wa kukeketa watoto wachanga unafanywa kwa uficho baina ya mama mzazi na baadhi ya Ngariba.

"Huwezi kubaini mapema kwani ni Siri wanafanya sisi tunawabaini watoto pale ambapo wanaumwa na kupelekwa Hospitali"alisema

Nashoni Mollel (si jina halisi)anasema kuwa mzazi wake alimkeketa mdogo wake akiwa mdogo kutokana na mila hiyo kuendelea na kutaka mtoto awe na heshima ya kuolewa.


"Hata Mimi nimekeketwa nikiwa mdogo lakini wazazi walifanya hivi ili niwe na hadhi ya kuolewa maana huku kwetu Kama hujakeketwa ni ngumu kupata mtu wa kukuoa"alisema.


Namnyaki Laizer amesema vitendo vya ukeketaji vimekuwa vikiendelea licha ya madhara ikiwepo kuugua ugonjwa wa festula.

"Mimi nilifanyiwa ukeketaji nikapata festula na Sasa nimekuwa natoa elimu kupinga ukeketaji," amesema kwa uchungu Namnyaki.

Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Longido, Grace Mghase amesema kuendelea kwa vitendo vya ukeketaji vinachangiwa na vijana kuwa wazito kuoa binti ambaye hajakeketwa.

"Hili Jambo bado linamizizi Sana sisi tunatoa elimu lakini ajabu kuna vijana na wasichana wenye elimu lakini bado wanaunga mkono ukeketaji,"alisema Mghase.
 
Alisema hata baadhi ya wanasiasa katika Wilaya hiyo bado wanaogopa Mila hii potofu kuipinga hadharani.

 
"Ni kweli tunataarifa wanakeketa watoto wachanga ili kukwepa kukamatwa lakini wajuwe serikali ina mkono mrefu tukiwabaini watakamatwa"alisemaò

Muelimisha Jamii, Mary Laizer, amesema kuwa wanaendelea na zoezi la kuelimisha jamii  kuwa kitendo  ukeketaji Wilaya ya Longido ina  madhara makubwa kwa wasichana na wanawake ikiwepo kupoteza maisha.

 "Mimi mwenyewe nilifanyiwa ukeketaji wazazi wangu Walikuwa hawajuwi athari zake lakini Sasa wamejua na Mimi nimekuwa natoa elimu kupinga ukeketaji,"alisema Laizer na kuongeza.

"Hivi Sasa wanahamasisha kuwavusha Rika watoto wa kike bila kuwakeketa lakini pia kutoa elimu kwa vijana kuacha Mila ya kupinga kuoa msichana ambaye hajakeketwa.

Mkurugenzi wa Shirika la TEMBO la Wilaya ya Longido mkoa Arusha, Pauline Sumayani alisema changamoto ya ukeketaji bado ipo lakini shirika lao linajitahidi kutoa elimu kupinga ukeketaji.


"Tunatoa elimu kwa wanawake,vijana na wazee kuacha ukeketaji na tumekuwa tukitoa zawadi kwa wazazi ambao wanawavusha Rika watoto bila kuwakeketa"alisema

 

Madhara ya Ukeketaji Ukeketaji una madhara makubwa kwa afya ya wanawake. Madhara ya kimwili yanaweza kuwa maumivu ya mara kwa mara, maambukizo, au hatari kubwa wakati wa kujifungua. 

Kisaikolojia, wanawake wanaopitia ukeketaji wanaweza kukumbwa na unyanyasaji wa kisaikolojia, wasiwasi, na hata shida za akili. Pia, mwanamke aliyekeketwa anaweza kupata matatizo ya kijinsia kama vile maumivu wakati wa tendo la ndoa.

Mbinu za Kuzuia Ukeketaji Serikali za mitaa na mashirika ya kijamii katika Mkoa wa Arusha zimechukua hatua za kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ukeketaji. 

Elimu hii inahusisha kutoa taarifa za kisayansi kuhusu madhara ya ukeketaji, na jinsi unavyoathiri afya ya wanawake. Viongozi wa kijamii wamewasiliana na wazee na wazazi katika jamii hizi, wakiwaeleza athari za ukeketaji na kujaribu kubadilisha mitazamo.


Kupambana na Ukeketaji Kupitia Sheria na Haki za Binadamu Sheria zinazopiga marufuku ukeketaji zinapaswa kutekelezwa kwa nguvu zote. 

Vyombo vya sheria vina jukumu la kuhakikisha kuwa wahusika wote wanawajibishwa kisheria kwa kukiuka sheria hizi. Haki za binadamu, pamoja na haki ya kuchagua kuhusu mwili, zinapaswa kulindwa kwa kila mwanamke na msichana.

Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji inatukumbusha umuhimu wa kupigania haki za wasichana na wanawake. 

Katika Mkoa wa Arusha, ni wakati wa kufanya jitihada za pamoja kuelimisha jamii na kuhakikisha kwamba mila hatari kama ukeketaji zinakoma. 

Kwa kufanya hivyo, tunaweza kujenga mazingira salama na bora kwa kizazi kijacho na kuhakikisha kwamba wanawake wa Mkoa wa Arusha wanapata nafasi ya kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya jamii zao. 

Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji ni mwanzo mzuri wa safari hii.


Katika utafiti wa kisayansi unaojumuisha machapisho kadhaa kama vile Tanzania Health and Demographic Survey 2020 na The Lancet Global Health, inathibitisha kuwa ukeketaji unaweza kuwa na madhara makubwa kwa afya ya wanawake. 

Hatua za kisheria na elimu ni muhimu katika kuzuia na kutokomeza ukeketaji katika jamii za Mkoa wa Arusha na mahali pengine.

0 Comments:

Post a Comment