AKIRI KUMKATA MKE KIGANJA, AFUNGWA MIAKA MINNE, FAINI MILIONI 15

Ombeni Alfayo (aliefunika sura na shuka ya kimasai) leo akiwasiliana na wakili wake, Richard Manyota


MAHAKAMA Kuu  Kanda ya Arusha imemhukumu, Ombeni Alphayo (35) kifungo cha miaka minne jela na kulipa fidia ya shilingi 15 milioni, baada ya kukiri kosa la kujaribu kumuua aliyekuwa mke wake Veronica Kidemi kwa kumkata kitu chenye ncha kali hivyo kutenganisha mkono na kiganja cha mkono wa kulia.



Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Februari 8, 2022
na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Jaji Joachim Tiganga, aliyekuwa akisikilza shauri hilo la jinai namba 30/202.


Amesema mtuhumiwa huyo amekiri  kutenda kosa hilo Septemba 25, 2020 nyumbani kwake, kinyume na kifungu cha 211 cha sheria ya kanuni ya adhabu, ambapo baada ya kuangalia hoja za pande zote na yeye mwenye kukiri kutenda makosa hayo mahakama imemtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka minne jela na kutakiwa kulipa fidia ya Sh15 milioni.

Jaji Tiganga amesema katika kutoa hukumu mahakama inatakiwa isiangalie ukubwa wa kosa pekee bali itazame shufaa zilizotolewa na mshtakiwa pamoja na kutumia busara na kuangalia iwapo ni mkosaji wa mara ya kwanza.

"Mahakama inaona mshtakiwa anatakiwa kuonewa huruma japo wakili wake aliomba apewe adhabu mbadala ila mahakama inaona adhabu mbadala haitatenda haki," amesema Jaji Tiganga na kuongeza.

....Mahakama inaona kwamba adhabu ya jela ndiyo adhabu mwafaka, hasa ikizingatia mshtakiwa anayo majukumu ambayo mahakama ya chini imempata ya kutunza familia hasa watoto,".

"Mahakama inatoa adhabu ya kifungo cha miaka minne jela na baada ya hapo kwa kuzingatia ukweli mhanga amepoteza kiungo inatoa amri ya fidia Sh15 milioni kwa mwathirika, nafahamu fedha huenda  isitibu wala isitoshe na kiungo cha binadamu hamna fedha inarejesha hiyo ni kifuta jasho, na kama kuna ambaye hajaridhika na uamuzi anaweza kukata rufaa,".

Kwenye kesi hiyo upande wa Jamhuri ulikuwa unawakilishwa na Mawakili wa Serikali, Grace Madikenya na Charles Kagirwa huku mshitakiwa, Ombeni  akiwakilishwa na Wakili Richard Manyota.

 
Mnamo Septemba 25, 2020 Ombeni alimkata mke wake, Veronica ambaye ni  Mwalimu wa Shule ya Sekondari Sokoni II na  kitu chenye ncha kali hivyo kutenganisha mkono na kiganja cha mkono wa kulia.

Tukio hilo lilitokea nyumba kwao maeneo ya Siwandeti kata ya Kimyaki wilayani Arumeru ambapo Ombeni ambaye ni mfanyakazi wa shirika la umeme nchini, (Tanesco) jijini Dar es Salaam alitoroka mara baada ya kutenda kosa hilo.

Hata hivyo jeshi la polisi lilifanikiwa kumkamata akiwa jijini Dar es Salaam ambapo alirejeshwa jijini Arusha na kufikishwa mahakamani ambapo leo aliamua kukiri mashtaka yake wakati shauri hilo lilipokuwa likiendelea kwa upande wa Jamhuri kuanza kuleta ushahidi wake.


0 Comments:

Post a Comment