SABAYA NGOMA NZITO, MAWAKILI WAKE WATINGA MAHAKAMA YA RUFANI

 


MAWAKILI wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake... wameenda mahakama ya rufani nchini wakiiomba kufanyia marejeo uamuzi mdogo na mwenendo wa kesi ya rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) dhidi ya wateja wao.


Hatua hiyo imesababisha shauri hilo la rufaa namba 155/2022 lililokuwa likiendelea kwenye mahakama Kuu ya Kanda ya Arusha mbele ya Jaji Fatma Maghimbi kusimama mpaka mahakama hiyo ya juu itakaposikiliza na kutoa uamuzi.

Rufaa hiyo dhidi ya Sabaya na wenzake watano inapinga hukumu iliyotolewa Juni 10, 2022 na Hakimu Mkazi Patricia Kisinda kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, ambapo aliwaachia huru Sabaya na wenzake sita katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2021.

Wakili wa Serikali waandamizi Felix Kwetukia aliieleza mahakama hiyo leo Jumatatu Februari 20, 2023 kuwa Februari 3, 2023 walipokea maombi ya kufanya mapitio yaliyoandaliwa Januari 27, 2023 yanayoomba Mahakama ya Rufani ifanye mapitio ya mwenendo wa rufaa hiyo na uamuzi mdogo uliotolewa Desemba 14, 2022.

"Kwa msingi huo kwa kuwa kuna maombi ya mapitio ni rai yetu rufaa hii isubiri kwa muda ikisibiri usikilizaji na uamuzi wa maombi ya upande wa wajibu rufaa yaliyopelekwa katika mahakama ya rufani," amesema Wakili wa Serikali Mwandamizi,  Kwetukia.

Kwa upande wake wakili wa wajibu rufani, Mosses Mahuna ameieleza mahakama hiyo kuwa anakubaliana na maombi ya upande wa jamhuri na kuwa hawana nyongeza.

Hata hivyo ameieleza mahakama hiyo kuwa mpaka sasa hawajui maombi hayo yamesajiliwa kwa namba ngapi ingawa wanataarifa kuwa kuwa yameshasajiliwa.

Jaji Maghimbi amesema kuwa shauri hilo litasismama mpaka maombi hayo ya marejeo  yaliyofunguliwa mahakama ya rufani yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Wajibu rufaa kwenye shauri hilo ni Sabaya, Enock Mnkeni, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Ambapo wajibu rufaa waliokuwa mahakamani hapo ni Sabaya na Mnkeni ambapo wajibu rufaa wawili Aweyo na Nyegu wakiwalilishwa na mawakili wao huku mawakili hao wakieleza mahakamani hapo hawana taarifa za wajibu rufaani, Msuya na Macha.

Upande wa jamhuri unawakilishwa na mawakili wa serikali waandamizi, Kwetukia, Timotheo Mmari na Hebel Kihaka huku upande wa wajibu rufaa ukiwakilishwa na mawakili Mahuna, Fauzia Mustapha, Fridolin Bwemelo na Sylvster Kahunduka.


Awali, Desemba 14, 2022 Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilitupilia mbali pingamizi lililokuwa limewasilishwa mahakamani hapo na mawakili wa mjibu rufani wa kwanza,  Sabaya.


Aidha mahakama hiyo ilitupilia mbali hoja ya rufaa hiyo kukatwa nje ya muda pamoja na ufafanuzi kuhusu mrufani wa tatu, Watson Mwahomanhe ambaye awali upande wa wajibu rufaa uliibua hoja ya kutokuonekana mahakamani.

Jaji Maghimbi alisema kuwa rufaa hiyo iliwasilishwa ndani ya wakati na kwa mujibu wa sheria ambapo siku 45 za kukata zinaanza kuhesabiwa pale nakala za mwenendo wa kesi na uamuzi unakuwa umetolewa.

Alisema anakubaliana na hoja ya wakili wa serikali mwandamizi Patrick Mwita ambaye wakati akijibu hoja za pingamizi hilo la awali aliileza mahakama kuwa siku 45 za kukata rufaa zinaanza kuhesabiwa baada ya kukabidhiwa nakala ya mwenendo wa kesi na hukumu.

Kuhusu hoja ya pili iliyotolewa na Mahuna akidai kuwa notisi ya nia ya kukata rufaa inatofautiana na maombi ya rufaa, Jaji alisema anakubaliana na hoja ya wakili wa serikali mwandamizi Patrick Mwita kuwa baada ya kupata mwenendo wa shauri na hukumu ndipo unaweza kuamua nani umkatie rufaa.





0 Comments:

Post a Comment