NIC YAWAFIDIA WAKULIMA SIHA ZAIDI YA SH 257 MILIONI


SHIRIKA la Bima la Taifa, (NIC), limetoa fidia ya zaidi ya shilingi milioni 257.3 kwa chama cha ushirika wa kilimo na masoko cha Nafaka (AMCOS) kufidia hasara waliyoipata kwenye msimu wa kilimo wa 2021/2022.


Wakulima hao walikopa benki ya NMB kiasi cha shilingi milioni 350 baada ya kukatia bima mazao yao ya ngano ambayo kutokana na ukame hawakupata mavuno ya kutosha ndipo bima ikawajibika kuwafidia hasara hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa NIC,  Dkt Elirehema Doriye, amekabidhi hundi hiyo leo Februari 17, 2023 kwa katibu wa Nafaka AMCOS, Bertho Mbilinyi akiwa ameambatana na baadhi ya wajumbe wa bodi na wanachama wa ushirika huo.


Mbilinyi amesema kuwa ushirika wao unaundwa na wanachama 318 ambao wanaendesha shughuli za kilimo kwenye kata ya Ngarenairobi wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.

Hata hivyo anasema kuwa wanachama walioridhi kukata bima ya mazao ni 16 tu ambao ndiyo watanufaika na maklpo hayo yaliyotolewa na NIC jambo alilosema kuwa hiyo itawafanya na wanachama wao wengine kuridhia kujiunga na mpango wa kukata bima ya mazao kwani wameuona una manufaa.

"Niwasihi wakulima wenzangu wa mazao wasisite kuitumia NIC kwa sababu sisi tuliweka bima kwa kazi za kilimo tunazofanya kwa kweli ni shirika zuri lina watendaji wazuri na wafuatiliaji. Walikuwa na sisi hatua kwa hatua kuanzia shamba mpaka hapa tulipofikia tunawashukuru sana na tunaahidi kuendelea kushirikiana nao,"amesisitiza Mbilinyi.


Akiongea mara baada ya kukabidhi hundi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Dkt Doriye amesema kuwa msimu wa 2021/2022 wakulima wa Nafaka AMCOS walifanya uwekezaji wa zaidi ya shilingi milioni 500 ambapo kutokana na ukame mkali hawakupata mavuno kama walivyotarajia hivyo walipata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 257. 

"Leo tumewakabidhi hundi ya shilingi milioni 257 kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa kilimo wa 2023/24 sanjari na kufidia hasara waliyopata kwenye msimu wa kilimo wa 2021/2022," amesema Dkt Doriye.

Amesema kuwa tayari wameshatoa elimu ya bima ya kilimo na mifugo kwa zaidi ya wafugaji elfu 10 ambapo kati ya hao tayari wakulima elfu 6 na wafugaji 1,000 wameshakata bima.

"NIC imeshatoa fidia ya zaidi ya shilingi milioni 300 kwa wakulima 6,000 na  wafugaji 1,000 kutokana na hasara walizopata kutokana na majanga ya kwenye shughuli zao na fedha hizi hazijumuishi hizi tulizotoa kwa Nafaka AMCOS leo," amesema Dkt Doriye na kuongeza

...Tunaendelea kutoa fidia kwa sababu mavuno huwa yanatofautiana msimu hadi msimu hivyo tunaendele kutoa fidia kwa wakulima na wafugaji kadiri wanavyoendelea kutoa taarifa kulingana na hasara walizopata,".

"Wakulima na wafugaji waelewe bima ya kilimo inalipa na inasaidia kuondoa 'stress' wanazoweza kupata na  kuwakatisha tamaa kwani unapotokea ukame mkali huua mifugo na kuharibu mazao hivyo kuharibu  malengo waliyotarajia lakini ukijiunga  na bima hauna haja ya kukata tamaa,".

 Mkurugenzi Mtendaji huyo wa NIC amesema kuwa majanga ya kiasili  huchangia kuwakatisha tamaa wakukima na wafugaji  kwani mitaji waliyo nayo mara nyingi huwa wamekopa benki au imetokana na shughuli zao za maisha za kila siku.

"Kwa kiasi kikubwa kilimo kimekuwa kikionekana ni sehemu ya kuwatia umaskini wakulima hivyo NIC  tumekuja kuwatoa hofu wananchi na wakulima," amesisitiza Dkt Doriye.

Amesema kuwa NIC ni taasisi ya serikali hivyo inawajibu wa kuhakikisha malengo ya serikali yanafikiwa ya kuhakikisha kilimo kinakuwa kwa asilimia 10 inapofika mwaka 2030 ambapo kiwango hicho cha ukuaji kitachangia kupunguza umasikini kwa asilimia 50. 



2022/23 serikali ilitenga zaidi ya shilingi bilioni 900 kwa ajili ya kilimo hivyo uwekezaji huu lazima ulindwe kupitia bima ambayo NIC kama taasisi ya kiserikali inatekeleza wajibu huo.

Kwenye bajeti ya kilimo ya 2022/2023 serikali imetenga jumla ya Sh751 bilioni sawa na asilimia 155.34 ikilinganishwa na Sh294 bilioni za bajeti ya mwaka 2021/2022 wa fedha ambapo ongezeko hilo ni karibu mara tatu ya bajeti ya mwaka uliopita .

 

NMB WASEMA KAMA SI NIC WANGEPATA HASARA KUBWA 



Meneja wa NMB tawi la Siha, Frank Kilas qmbao ndiyo walitoa mkopo huo amesema kuwa walipoanza mchakato wa kukatia bima wakulime wengine walikuwa wagumu kuelewa isipokuwa Nafaka AMCOS wenyewe walibali kukata bima ya mazao hivyo wakawakopesha fedha za kulimia zao la ngano.

"Kwa tukio la wakulima hao kufidiwa na NIC inapeleka ujumbe mzito kwa wakulima wengine kuelewa kuwa wanapokata bima ya mazao wanaweza kufidiwa endapo yatatokea majanga ya asili yatakayowasababishia hasara kwenye kilimo,"

Kilas alisema kuwa NMB inafanya kazi na makampuni 10 ya bima ikiwemo NIC katika kukatia bima mbalimbali ikiwemo bima za kilimo, magari,  nyumba na nyinginezo.

"Kwa hili la leo niwashukuru sana NIC, kwa sababu hasara ambayo tungeenda kupata kutokana na ukame wa msimu uliopita ilikuwa ni kubwa sana ingeweza kuturudisha wote shimoni lakini bima imeturudisha wote shambani tukiwa tunacheka mambo yetu yanakwenda vizuri 
," amesema Kilasi na kuongeza

...Msimu unaokuja unaoanza mwezi Machi wote tunakwenda kifua mbele kumkopesha mkulima kwa sababu tunajua mazao yake yatakuwa yamekatiwa bima,".



Kwa upande wake, Meneja wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko,(CPB) Kanda ya Kaskazini, Peter Mobe, aliwahimiza wakulima wa mazao ya nafaka kukatia bima mazao yao ili inapotokea majanga waweze kufidiwa.

Alisema kuwa wao wamekuwa wakifanya kilimo cha mkataba na wakulima ambapo kwenye Nafaka  AMCOS  waliwapatia mbegu za ngano ambapo walipanda lakini kutokana na majanga ya ukame walipata hasara. 

"Sisi tumefarijika baada ya kuona NIC imewapa fidia waliopata hasara hii italeta chachu kwa wakulima wengine kukatia bima mazao yao ili majanga yakitokea na kushindwa kupata mavuno ya kutosha NIC iwafidie kama ilivyofanya hapa," alisema Mombe.

Awali 2020 CPB walikuja na mpango kabambe wa kufufua zao la ngano nchino ambapo mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo ya serikali, Dkt Anslem Moshi alikutana na wakulima wa ngano kwenye mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara ambapo baada ya mazungumzo ya muda mrefu walifikia makubaliano ya kuendesha kilimo cha mkataba.


CPB iliwakopesha wakulima hao mbegu za ngano ambazo ziliingizwa nchini na kampuni ya mbegu ya Seed Co baada ya mbegu hizo kukidhi viwango vya ubora ambapo baada ya mavuno wakulima hao waliuza mazao yao kwa CPB pamoja na kulipa deni la mbegu.

Hata hivyo kutokana na wakulima hao kuwa wanaendesha kilimo cha kutegemea mvua hali ya hewa haikuwa nzuri hivyo hakukuwa na mvua za kutosha kwenye maeneo mengi hali iliyopelekea baadhi ya wakulima kutopata mavuno ya kutosha hivyo kupata hasara.



0 Comments:

Post a Comment