UKITAKA KUFANIKIWA LAZIMA ULE PILIPILI MWAKA MMOJA

 

" Mjasiriamali lazima ule pilipili mwaka mmoja ndiyo utaona matunda ya kazi yako baada ya hapo unaweza kula sukari bila wasiwasi," .


Hayo ni maneno yaliyobeba maana kubwa sana anayosema Nailejileji Mollel kwa kila anayepita kwenye banda lake la lililopo maonyesho yanayoendelea  kwenye uwanja wa TBA jijini Arusha.
  

Maonyesho hayo ya Kanda ya Kaskazini yameandaliwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo, (SIDO) kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha yaliyoanza Oktoba 19, 2022 yanategemewa kuhitiishwa Oktoba 25, 2022 .

Mollel ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Esidai anauza bidhaa mbalimbali anazotengeneza ikiwemo sabuni ya maji ya kuoshea nywele(shampoo) inayoonyesha kupendwa na watu wengi kutokana na namna inavyosaidia nywele kuwa ndefu na zenye muonekano mzuri.



Bidhaa nyingine anazouza ni pamoja na sabuni za maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, mafuta ya kujipaka, lotion za watoto na wakubwa, vikapu vya shanga na batiki.

Mwana mama huyo kutoka jamii ya wafugaji mbali na kutengeneza na kuuza bidhaa hizo lakini pia anajitolea kufundisha wananchi wanaotoka kwenye mazingira magumu anahamasisha watu kutumia muda wao vizuri kwa kuwa na ratiba maalum.

" Huwezi kufanikiwa kama hauna ratiba ya siku mimi nalala saa nane usiku naamka saa 10.59 asubuhi kila siku na natumia saa moja kufanya maombi," anasema Mollel na kuongeza

... saa 12 mpaka saa 3 asubuhi anatumia kwa ajili ya kutembeza kuuza vitafunwa vyake ambapo saa nne mpaka saa saa 5 asubuhi anatembeza mbogamboga huku saa nane mchana mpaka saa 11 jioni akiutumia kutembeza nguo na viatu,".

Mollel anasisitiza kuwa watu wakimaliza kazi hupenda kuongeaongea hivyo yeye hutumia muda huo kuwauzia bidhaa zake.

Hata hivyo anasema kama mama wa familia anajua majukumu yake ya kuihudumia familia yake kwa kuhakikisha wanapata mlo bora kwa wakati ambapo kuanzia saa 12 mpaka saa 2 usiku anaandaa chakula na kuhakikisha familia yake ya yenye watoto wanne inakula lwa wakati.

Mollel ambaye ni mchangamfu anayeongea akitabasamu muda wote anasema kuwa saa 2 mpaka saa 3 usiku huangalia taarifa ya habari kujua mambo yanayoendelea ndani na nje ya nchi.

 " Ili kufanikiwa kwenye kazi zako ni lazima kumweka Mungu mbele. Mimi nahakikisha napata muda wa kutosha kwa ajili ya sala na maombi kwa Mungua kuanzia saa 3 usiku mpaka saa nne nasali nilizingafia MITHALI 3:3," anasema Mollel na kuongeza 

... kuanzia saa 4 usiku mpaka saa 7:59 usiku natengeneza bidhaa zangu kwa ajili ya kwenda kuuza siu inayofuata. Utaona ninalala saa tatu tu zinatosha kabisa mjasiriamali unatakiwa kutumia muda vizuri ukiona mafanikio hapo unaweza kulala hizo saa nane wanazaoshauri wataalam,'.


Mwanamama huyo ambaye ofisi zake ziko Loksale wilayani Monduli mkoani Arusha na nyingine ziko Simanjiro mkoani Manyara anasema kuwa akishawapatia mafunzo watu hao kutika kwenye mazingira magumu pamoja na walemavu huwapa fedha  kwa ajili ya kuanzisha biashara kati ya shilingi 5,000 na 30,000 ambazo hawatakiwi kuzirejesha.

"Kuanzia kwa 1995 nilipoanza kutoa mafunzo haya ya ujasiriamali nimeshatoa mafunzo kwa watu 14,000. Nimetoa za mtaji kwa watu 2,000 ili waweze kutumia mafunzo niliyowapa kuzalisha bidhaa zao wenyewe," anasema Mollel.

Hata hivyo anasema kuwa changamoto anayokumbana nayi ni kuwa wanawake wengi wa jamii ya wafugaji wanakuwa wazito kupokea jambo mpaka pale wanapoona kuna waliofanikiwa ndipo wengi hujitokeza kujifunza.

"Najivunia kuona watu niliowafundisha wakiwa wamefanikiwa. Wengine wametajirika wanafedha nyingi kuliko hata mimi wakinikuta huwa tunasalimiana kwa upendo hiyo inanipa faraja sana," anasema Mollel huku tabasamu likiwa limeujaa uso wake.




0 Comments:

Post a Comment