DC RUYANGO AISIFU SHULE YA TURKISH MAARIF KUKUZA VIPAJI VYA WANAFUNZI

 

MKUU wa wilaya ya Arumeru, Mhandisi, Richard Ruyango amesema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji toka nje kwani matunda yanaonekana kwenye sekta mbalimbali ikiwemo elimu ambapo shule ya kimataifa ya Turkish Maarif inayomilikiwa na serikali ya Uturuki inafanya vizuri kwa kutoa elimu bora.


Aidha amepongeza hatua ya shule hiyo kuweka msisitizo kuendeleza vipaji vya watoto kwa kuwawezesha kutimiza ndoto zao kwa yale wanayoyajua nje ya masomo ambapo mmoja wa wanafunzi hao alionyesha ndege aliyoitengeza ambayo ametumia kemikali rafiki na mazingira kuirusha.


Ameyasema hayo leo Oktoba 22,2022  wakati wa mahafali ya wanafunzi 87 wa  chekechea, msingi na sekondari ya shule za Turkish Maarif iliyopo Ngaramtoni wilayani Arumeru, mkoani Arusha. 


"Serikali inavyofanya kazi na wawekezaji shule hii inaendeshwa na serikali ya Uturuki na inayoa elimu bora kwa vijana wetu. Rais Samia Suluhu Hassan mara zote anatuhimiza tuhakikishe kila wakati tunawapa ushirikiano wawekezaji na hii ndiyo faida," amesema Mhandisi Ruyango na kuongeza

....Tumeona ni jinsi gani vijana wetu wana vipaji mbalimbali  wanaweza kuongea lugha nne kwa wakati mmoja, (Kiswahili, Kiingereza, Kirafansa na Kituruki) vijana wa chekechea wameweza kuimba nyimbo za asili za Tanzania, vijana wa sekondari wameimba Kituruki,".


"Niwapongeze shule hii kwa mazingira mazuri, majengo mazuri na waalimu wanavyowafundisha watoto vizuri na hii inadhihiridhwa na yale watoto waliyotuonyesha hapa.

Wazazi mtakubaliana na mimi watoto wenu wanaohitimu hapa wana mabadiliko makubwa kimakuzi na kielimu,".

Hata hivyo aliwakumbusha wazazi suala la malezi ya watoto ni la waalimu na wazazi ambapo aliwaambia ni vema wakatimiza wajibu wao badala ya kuacha jukumu hilo kwa waalimu pekee.


"Watoto wameniambia wametumia shilingi 100,000  kwa ajili ya kuandaa 'jet' (ndege) nawarudishia ili waendelee na utafiti wao  lengo langu ni kuwafanya vijana hawa wasikate tamaa waendelee kuwa wabunifu," amesema mhandisi, Ruyango.


Mkurugenzi wa shule hiyo, Halil Server amesema wanaendelea kuboresha miundo mbinu ya shule hiyo ikiwemo kupanua bwalo la kulia chakula na chumba cha tehama ili viweze kutumiwa na wanafunzi wengi zaidi kwa wakati mmoja.



Kwa upande wake, Mwalimu mkuu wa Turkish Maarif msingi, Rafael Sabaya amewasihi  wazazi kubadili mtazamo wa kutaka watoto wao kusoma ili wafanye kazi za kuajiriwa tu badala yake wawaache watumie vipaji walivyonavyo kujitengenezea ajira.

"Sisi tunaamini katika elimu kwa vitendo kwa sababu kuna vijana wengi wamesoma vizuri lakini wako nyumbani kwa kukosa ajira. Katika kutoa elimu kwa vitendo vijana wengi wataweza kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa," amesema mwalimu Sabaya na kuongeza.


" Zaidi ya elimu ya darasani watoto wenye vipaji tunawasaidia wavitimize. Kama mtoto ana kipaji cha mpira mwache aende hukohuko, kama ana kipaji cha kuchora mwelekeze hukohuko inawezejana ndiyo talanta yake Mungu aliyompa mwache aiendeleze,".
 


Awali akisoma risala kwa niaba ya wahitimu, Ethan amesema shule hiyo imewapa elimu bora itakayowawezesha kukabiliana na mazingira yao na kuweza kuishi na jamii.


Akiongea kwa niaba ya wazazi wa wahitimu, Vivian Lobulu aliwatia moyo watoto hao kwa kuwataka wasikate tamaa wajitume kusoma watapata matokeo mazuri.

Aidha aliwashukuru waalimu kwa malezi na elimu waliyowapa watoto hao kwa miaka minne waliyokuwa hapo shuleni.


 

0 Comments:

Post a Comment