MALKIA Maxima wa
Uholanzi ameelezea kuridhishwa na namna taasisi ya kutengeneza bima ya mazao na
mifugo,(ACRE Afrika) nchini Tanzania ilivyowawezesha wakulima kupata
fidia ya mazao kutokana na janga la ukame kupitia 'bima pima'.
Ameyasema hayo leo, Oktoba 18, 2022 wakati akijadiliana na wakulima wa mahindi kwenye Chama Cha Msingi Cha
Ushirika cha Uduru Makoa kilichopo Kata ya Machame Kaskazini, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.
Malkia Maxima ambaye
alionekana kuuliza maswali mengi wakulima hao ameelezea kufurahishwa na namna
ambavyo wakulima hao wanaelezea kunufaika na bima hiyo huku akishauri mifumo
hiyo ya bima iboreshwe zaidi ili iweze kuwafikia wakulima wengi zaidi.
Kwenye majadiliano hayo
Mkulima mhamasishaji, Cleopa Mushi ambaye alishiriki kuhamasisha wakulima
kununua vocha (bima) ili kukabiliana na majanga ya ukame na uhaba wa mvua
amesema kuwa msimu ujao yeye na wakulima wenzake wamejipanga kununua vocha
nyingi zaidi kwani wameona mafanio yake.
"Nimewahi kupata
malipo ya bima ya shilingi 120,000, mimi nimeona faida ya huu mradi kwa sababu
hizo fedha nilitumiwa kwenye simu yangu wakati wa maandalizi ya msimu
mwingine wa kilimo. Hivyo ikanisaidia kwa sababu msimu iliopita nilikuwa
sijapata mavuno vizuri hivyo ingenilazimu kwenda kuuza vitu vingine ili niweze
kuanza kuandaa shamba lakini malipo ya boma ya ACRE Afrika yamenisaidia
sana," amesema Mushi.
Mkulima mwingine Irene
Ndenshao alisema kuwa yeye alinunua vocha moja ambayo inauzwa shilingi elfu
moja kwa hofu kuwa huenda anaweza kutapeliwa hivyo baada ya msimu kuisha mavuno
hayakuwa mazuri.
" Nilishangaa kuona
natumiwa shilingi 12,000 kwenye simu yangu nikashangaa sana kwa sababu nilikuwa
nimesahau kama nilikuwa nimekata bima ya mazao hivyo kwenye msimu huu nimepanga
kununua vocha nyingi zaidi," alisema Ndenshao.
Akimkaribisha Malkia
Maxima kuzungumza na wakulima hao, Mkurugenzi wa kampuni ya Acre Afrika, nchini
Tanzania, Chrisopher Mazali alisema kuwa wanatekeleza mpango wa wa kutengeneza
bima hapa nchini kuanzia mwaka 2015 ambapo wameanza na mikoa ya kilimanjaro na
Arusha.
"Ujio wa Malkia
Maxima hapa kwenye kata ya Uduru ulikuwa ni kuja kujifunza huduma ya bima ya
mazao tunayotoa kwa wakulima wa mahindi ambapo miradi kama hii
tunaisimamia kwenye wilaya za Siha mkoani Kilimanjato na Arumeru mkoani
Arusha," alisema Mazali na kuongeza.
...Bima tunayotoa kwa
wakulima wadogo inaitwa 'bima pima' ni bima tunayoitoa kwa mfumo wa vocha
ambayo imelenga kuwatambulisha wakulima mfumo wa bima ambapo vocha moja inauzwa
shilingi elfu moja.
Hii inalinda gharama za
uwekezaji za mpaka shilingi 12,000 kwa kadi moja hivyo mkulima akipata hasara
anaweza kulipwa fidia mpaka shilingi 12,000 ambapo mkulima anaweza kununua
vocha zaidi ya moja kulingana na gharama anayotaka kuilinda kwenye kilimo
chake,".
Mazali alisema kuwa wameanza
kuendesha shughuli zao nchini kuanzia mwaka 2015 ambapo wamekuwa wakitumia
wakulima wahamasishaji kuwaelimisha umuhimu wa bima hiyo inayolipa majanga ya
ukame na mvua nyingi inayoharibu mazao.
"Tumejipanga kutoa
bima kwa wakulima laki moja kwenye msimu ujao wa kilimo na tutafanya hivyo
kwenye mikoa saba nchini. Mbali ya mahindi tutaangalia na mazao mengine kama
alizeti, pamba, kahawa,tumbaku na mazao mengine yanayokabiliwa na changamoto ya
mabadiliko ya tabianchi," alisema Mzali.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Kampuni ya mbegu ya SeedCo, kanda ya Afrika Mashariki, Clive
Mugadza alisema kuwa wamejikita kuzalisha mbegu zinazohimili changamoto za
tabianchi hivyo kuwawezesha wakulima kupata mavuno mengi na bora.
" Tunawashauri
wakulima kujiunga na bima ya kilimo kwani inapotokea majanga yanayoweza
kuwasababisha wasipate mavuno ikiwemo upungufu wa mvua basi waweze kupata
fidia ikiwemo kupatiwa bure mfuko wa mbegu za mahidi kwa ajili ya msimu
unaofuata," alisistiza Mugadza.
Naye Meneja Mkuu wa Bima, benki
ya CRDB, Wilson Mzava alisema kuwa wanashirikiana na taasisi ya ACRE
Afrika wameandaa mpango mzuri sana wa bima ya kilimo inayotoa fidia kwa
wakulima pindi wanapokumbwa na majanga.
"Bima ya mazao
inayotolewa benki ya CRDB inaongeza uhakika wa chakula nchini pia inamuongezea
mkulima uhakika wa kipato hivyo tunawashauri wakulima wengi kujiunga na bima
hii,' alisema Mzava.
Mmoja wa wakulima
alimweleza Malkia Maxima kuwa wameona mafanikio makubwa kupitia bima hiyo kwani
imewawezesha kuhama kutoka kilimo cha mbegu za kienyeji ambacho kwenye ekari
moja walikuwa wanapata gunia nne za kilo 100 kila moja ambapo kwa sasa
wananunua mbegu za kampuni ya SeedCo zinazowawezesha kupata wastani wa
magunia 25 mpaka 40 kwa ekari.
0 Comments:
Post a Comment