SHIRIKA lisilo la
Kiserikali la Maendeleo na Msaada la kanisa Katoliki Jimbo Kuu Arusha, (AAIDRO),
limeanza kutekeleza mradi wa zaidi ya shilingi milioni 230 kwa ajili
kusaidia kuwainua kiuchumi wanawake, kuwapa elimu ya ujasiriamali
na namna ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia.
Mkurugezi Mtendaji wa
AAIDRO, Padri, Faustine Mosha ameyasema hayo katikati ya mwezi huu wakati akimweleza Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Arusha, Seleman Msumi juu ya utekelezaji wa mradi huo wa mwaka
mmoja akiwa ameambatana na uongozi wa taasisi hiyo.
Amesema kuwa mradi huo
wa majaribio umelenga kuwanufaisha wananchi 200 ambapo Kanisa limeona ni vema kushirikiana na
Serikali kuwahudumia wananchi katika sekta nyingine zaidi ya ile ya kiroho na
kuongeza kuwa wanatarajia kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa watalamu wa
halmashauri ili kutekeleza mradi huo ipasavyo.
Padri Mosha amesema
kuwa idara ya maendeleo waliona ni vema wakapanua wigo kwa kuyaangalia makundi
ya kijamii ya kimkakati ikiwemo wanawake hasa kipindi hiki cha kuelekea
jubilei ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa jimbo kuu la Arusha ambayo
itaadhimishwa kuanzia mwakani mwezi machi.
“Tukampata huyo mhisani kutoka Ujerumani anayeitwa Misereor ambapo wamekubali kuwasaidia wanawake rasilimali fedha na ujuzi kidogo ili kuhakikisha idara hiyo ya kinamama inaweza kuwasaidia wanawake kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha kujitambua katika suala zima la maendeleo ya jamii,” amesema Padri Mosha na kuongeza.
…Tukaona tulenge
katika mkakati wa kuona wanawake wanatambua vizuri masuala ya haki zao,
wanashirikishwa vizuti katika kutambua rasilimali walizonazo na namna ya
kuzitumia na wao wenyewe kujitambua hivyo kuweze kuchochea maendeleo endelevu
kwa mwanamke mmoja mmoja na jamii kwa ujumla,”.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Msumi, amelishukuru Kanisa Katoliki
na AAIDRO kwa kuona umuhimu wa kuunga mkono juhudi za serikali za
kuwajengea uwezo wananchi kujikwamua kiuchumi, kazi ambayo ingefanywa na
serikali.
“Kama Hamashauri tuko
tayari kushirikiana na kanisa kwa kuzingatia jukumu la serikali ni kuweka
mazingira rafiki kwa mashirika yanayofanya kazi za kuhudumia jamii kulingana na
mpango mkakati wa serikali, tunao watalamu wa kutosha katika idara zote, hivyo
watashirikiana nanyi katika hatua zote za utekelezaji wa mradi huu,” amesema
Mkurugenzi huyo wa halmashauri ya Arusha.
Kwa upande wake
mratibu wa mradi huo, Irene Mosha, Amesema mradi huo uko chini ya Idara na Mradi wa wanawake na
Maendeleo, (WIDGAD) ambapo utawawezesha wanawake kiuchumi katika
masuala ya kilimo, kukuza biashara zao, usawa wa kijinsia, kupinga ukatili kwa
wanawake ikiwemo ndoa za utotoni na mambo mengine yanayofanana na hayo.
Amesema kuwa mradi huo
utawanufaisha wananchi wa kata za Nduruma na Bwawani kwenye vijiji vya Mzimuni,
Kigongoni Themi ya Simba na Bwawani ambapo utatekelezwa kwenye awamu tatu
na kwa sasa uko katika
hatua za awali ukitarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2023.
“Kupitia mradi
huu tunategemea kuwaiwezesha jamii kuwa na uwezo wa kujikomboa kifkra, uwezo wa
kujitegemea kiuchumi katika kujipatia pato la familia, pamoja na kuwa na jamii
huru isiyokuwa na ukatili wa aina yoyote katika masuala ya kijinsia,” amesema
Moshi.
Mtaalam Mshauri wa
AAIDRO, Rafael Kajuna amesema kuwa wamekuwa na miradi kadhaa ya kusaidia
wananchi waliyowahi kuitekeleza kwenye maeneo ambayo waliridhishwa kwa namna
wananchi walivyoipokea na kuiendeleza ndiyo sababu wakaona ni vema wakaelekeza
miradi mingine kwenye maeneo hayo.
Mjumbe wa bodi ya
AAIDRO, Isaya Doita amewasihi watendaji mradi huo na wale halmashauri
wafanye kazi iliyokusudiwa kwa uaminifu ili kuwezesha kufikiwa malengo
yatakayosaidia kupatikana kwa mtafi mkubwa utakaowanufaisha wananchi wengi
zaidi.
0 Comments:
Post a Comment